Wednesday 1 March 2017

WANAOWACHAFUA, KUWAKASHIFU WENZAO MITANDAONI KUKIONA CHA MOTO


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimesema wakati wa kuvumilia baadhi ya viongozi, watendaji na wanachama wanaowachafua na kuwakashfu wenzao kupitia mitandao ya kijamii umekwisha, badala yake kinaandaa taratibu za kuwachukulia hatua kali za kinidhamu  wanaohusika na vitendo hivyo.

Msimamo huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, wakati akizungumza na viongozi, watendaji na wafuasi wa Chama katika jimbo la Malindi, katika ziara ya siku 10 ya kukiimarisha katika mkoa wa mjini kichama

Amesema CCM kwa sasa inaandaa utaratibu kupitia vikao vyake vya kikanuni, kuwaita baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na tabia hizo ili kuwahoji na kuwapa nafasi ya kujitetea kabla ya vikao vinavyosimamia maadili kuchukua hatua za kinidhamu kwa watakaokutwa na hatia.

Vuai alisema taasisi hiyo imekuwa ikitoa onyo na tahadhari mara kwa mara ili watu wenye tabia hizo waache, lakini baadhi yao hawataki kubadilika, hali ambayo hawawezi kuivumilia kwa lengo la kulinda heshima na hadhi ya CCM na serikali zilizopo madarakani.

Alitoa ufafanuzi huo, kufuatia kusambazwa kwa habari za upotoshaji katika mitandao ya kijamii, zilizokuwa zikidai kuwa, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amevunja Baraza la Wawakilishi.

Alisema uvumi huo ulisababisha baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM, kuandika maneno yasiyofaa, wakiwashutumu viongozi wenzao ndani ya Chama kinyume na utaratibu.

Alitoa wito kwa wafuasi wa CCM na wananchi kwa ujumla, kufahamu kuwa  Chama na Serikali ni mamlaka kuu za nchi, hivyo zina utaratibu wake maalumu wa kutoa taarifa mbalimbali,  ambao ni rasmi na sio kupitia mitandao ya kijamii.

“CCM ni chama kinachoongozwa na katiba, maadili na taratibu, hivyo kila jambo lina utaratibu wake na hata suala la kukosoana ni lazima tufuate miongozo ya kikanuni, sio kudhalilishana katika mitandao ya kijamii na sehemu zingine zisizofaa kujadiliwa masuala ya Chama.

"Kabla hatujawachukulia hatua stahiki watu wanaokiuka miongozo yetu ya Chama, kuna hatari ya kutugawa na inawezekana wanatumiwa na vyama vya upinzani kutengeneza mpasuko na mimi nikiwa mtendaji  mkuu wa CCM Zanzibar, sitowavumilia tena, “ alifafanua Vuai.

Amewasihi wafuasi wa CCM kuwa na tahadhari juu taarifa za upotoshwaji zinazotolewa na vikundi vinavyoandaliwa na vyama vya upinzani, kwani zina nia ya kuwagawa wanachama ili washughulikie  propaganda hizo, badala ya kujiandaa na uchaguzi ujao wa Chama, unaotarajia kufanyika mwaka huu.

Alisema baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kususia uchaguzi wa marudio na kushindwa, kimekuwa kikitumia njia nyingine ya kuwaaminisha uongo na kuwahadaa wafuasi wao, mambo ambayo sio sahihi kupitia mitandao ya kijamii.

Alilitaka Jeshi la Polisi Zanzibar, kuwatafuta watu wanaomiliki na kusambaza taarifa za uongo kupitia mitandao ya kijamii, kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria kabla hawajaiingiza nchi katika machafuko.

No comments:

Post a Comment