Friday 3 March 2017

JPM: MARUFUKU KUSAFIRISHA MCHANGA WA MADINI NJE

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amezuia usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda kuuchenjua nje ya nchi, akitaka shughuli hizo zifanyike nchini.

Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kutengeneza vigae cha Tanzania Goodwill Ceramic, jana, Rais Magufuli alisema uchenjuaji wa mchanga wa madini nje ya nchi, unaikosesha serikali mapato, ikiwa ni pamoja na wizi madini hayo.

"Ndio maana nilikataa kusaini mkataba wa EPA, kwa sababu kupitia mkataba huo, ni vigumu kwa kampuni za Tanzania kushinda zabuni katika nchi za Ulaya, lakini ni rahisi kwa kampuni za Ulaya kushinda zabuni Tanzania, kutokana na kukomaa kiteknolojia. Na hata zinaposhindanishwa kampuni za Tanzania na Ulaya, ni rahisi kwa kampuni za Ulaya kushinda, jambo litakalochangia kuua kampuni zetu,”alisema Rais Magufuli.

Alisema Tanzania ni mwananchama wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki na nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo kujengwa kwa kiwanda hicho kutakiwezesha kiwanda hicho kunufaika kiuchumi.

Rais Magufuli alisema kwa muda mrefu, wawekezaji wamekuwa wakisafirisha malighafi za Tanzania nje ya nchi kwa ajili ya uzalishaji na kusababisha wananchi kutumia bidhaa zisizo na ubora.

Katika uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda hicho, Rais Magufuli alisema imefika wakati kwa Tanzania kuuza bidhaa zinazozalishwa viwandani na kuachana na kusafirisha malighafi nje ya nchi kwa ajili ya uzalishaji.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amesema serikali yake haina chakula cha kuwapa wananchi wanaopatwa na tatizo la njaa, badala yake amewataka kufanyakazi kwa bidii, ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha.

Awali, akitoa salamu zake kwa Rais Magufuli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Adelhelm Meru, alisema kujengwa kwa kiwanda hicho ni faida kwa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Naye Balozi wa China nchini, Lu Youqing, alisema Serikali ya China kwa sasa iko katika mkakati wa kuhamishia viwanda vyake vingi barani Afrika na imeamua kuichagua Tanzania kuwa moja kati ya nchi watakazohamishia viwanda hivyo, kutokana na kuridhishwa na dhamira inayoonyeshwa na serikali katika kuleta maendeleo.

Alisema China inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za kujikomboa, hivyo itaendelea kuiunga mkono kuhakikisha inafikia uchumi mzuri.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameziagiza kamati za ulinzi na usalama za mikoa nchi nzima kuhakikisha zinamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji.

Pia, alisema sehemu ambako bado kuna migogoro ya wakulima na wafugaji, watendaji kwenye maeneo hayo wajue hawafanyi kazi ya kuhakikisha kunakuwepo na ulinzi na amani.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo kwenye ziara yake ya siku nne katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, ambapo ziara hiyo alianzia mkoani Pwani katika wilaya ya Mkuranga.

Akiwa mkoani Lindi, katika eneo la Somanga, Kilwa, alisema anasikitishwa na migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kuwa ina hatarisha amani na imekuwa ya kila siku.

Rais Magufuli alisema anataka awaongoze Watanzania kwa amani na utulivu na hayuko tayari kuwepo kwa chokochoko zinazotokana na migogoro isiyokwisha ya wakulima na wafugaji.

Alisema kuanzia sasa ni marufuku kwa mfugaji kumnyanyasa mkulima na mkulima kumnyanyasa mfugaji na kuwa kila mtu anapaswa kuheshimiwa.

1 comment:

  1. Enter your comment...good our president!, let God fill you with leading power,follow what God guides you to do because he is the one who is perfect.

    ReplyDelete