Friday, 14 April 2017

AHADI ZA SERIKALI YA MKOA WA DAR ES SALAAM ZAZIDI KUKAMILIKA.





Makonda atembelea hospitali ya Koica Chanika leo jijini Dar es Salaam.

Hospitali ya Koica Chanika ya Mama na Mtoto inatarajia kuzinduliwa Juni mwaka huu, ambayo inawezo kuendesha oparesheni nne kwa siku.

Hospitali hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini ambapo kujengwa hospitali hiyo kulitokana na ombi la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokutana na Balozi wa Korea Kusini nchini.

Akizungumza wakati alipotembea hospitali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa hospitali hiyo ni mkombozi kwa wanawake na watoto kutokana na kuwa vifaa vya kisasa.

Amesema azma ya serikali ya awamu ya tano ni ya kuhakikisha wananchi wanyonge na masikini wanapata huduma za afya zilizo bora inatimia.

Makonda amesema hakuna kitu kinachoshindikana kama viongozi kufanya kazi za kujitoa kwa wananchi hasa katika sekta ya afya ambayo ndio msingi wa maisha ya watanzania.

Amesema hospitali hiyo ina hadhi yake kutokana na kuwa na vifaa vya kila aina zote ambapo hakuna mama atakayepoteza maisha kutokana na kujifungua ikitokea ni mipango ya Mungu.

Makonda amesema wanawake wakiwa na ujauzito walikuwa wanafikiri huduma wakati wa kujifungua lakini serikali ya awamu ya tano imeweka kipaumbele chini ya Rais wa Awamu ya Tano, Dk.John Pombe Magufuli.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema kuwa kujengwa kwa hospitali hiyo kutapunguza msongamano katika hospitali ya Amana.Amesema kutokana na vifaa huduma ambazo zitatolewa katika Hospitali hiyo kwa mama na mtoto zitakuwa ni za kiwango cha juu.

Mkuu wa Wilaya , Mjema amesema kuwa moja huduma hizo ni kuwa na mashine za kisasa za kufulia ambazo zinaweza kufua kilo 70 kwa saa.

No comments:

Post a Comment