Friday, 14 April 2017

WATANZANIA WANANE WALIOKUWA WAKISHIKILIWA NCHINI MALAWI WAACHIWA HURU

NA K-VIS BLOG NA MASHIRIKA YA HABARI

WATANZANIA wanane waliokuwa kizuizini nchini Malawi wakituhumiwa kufanya “ushushushu” wameachiliwa huru leo Aprili 13, 2017 na mahakama moja kwenye mji wa Mzuzu nchini humo.

Taarifa za vyombo vya habari vya Malawi zinasema, Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Muzuzi nchini Malawi, amewaachia huru Watanzania hao waliotiwa mbaroni Desemba 20, 2016 kwa tuhuma za kufanya “ushushushu” kwenye mgodi wa madini ya Urani wa Kayekera huko Karonga.

 Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Watanzania hao walikuwa wakishtakiwa kwa kosa la kuingia maeneo ya mgodi bila kibali ikiwa ni pamoja na shikata la kufanya “upelelezi”.


Hata hivyo Watanzania hao walikanusha mashtaka hayo tangu walipotiwa mbaroni.

Kwa mujibu wa Watanzania hao, sababu kuu iliyowafanya kufika kwenye eneo hilo ilikuwa ni ziara ya kimafunzo na wala haikuwa kufanya upelelezi kama ambavyo mamlaka za Malawi zilivyowatuhumu.

Baada ya Watanzania hao kupatikana na hatia, Hakimu huyo Mkuu Mkazi wa mahakama ya Muzuzu, Texious Masoamphambe, aliwahukumu Watanzania hao kifungo cha mwezi mmoja jela kwa kosa la kuingia eneo hilo bila kibali na kifu ngo cha miezi mitatu jela kwa kosa la kufanya “Ushushushu”

Hata hivyo Hakimu huyo aliitupilia mbali hukumu hiyo na kutoa sharti la watu hao kutofanya kosa katika kipindi cha miezi sita. Pia mahakama hiyo iliiamuru serikali kuwafukuza nchini Watanzania hao.

Aidha kuachiwa huru kwa Watanzania hao ambao tayari walikuwa wamekwisha hukumiwa kunatokana na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea baina ya Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ambapo Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt.Augustine Mahiga, alinukuliwa wiki iliyopita akitoa hakikisho la kuachiwa huru kwa Watanzania hao.

No comments:

Post a Comment