Sunday 23 April 2017

CHANGAMOTO ZA MUUNGANO ZATATULIWA KWA KIASI KIKUBWA : MAKAMBA


Na; Evelyn Mkokoi na Lulu Mussa – Dodoma

Waziri wa Nchi anayeshughulia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. January  Makamba, amesema kuwa changamoto za Muungano wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar zimetatuliwa kwa kiasi kikubwa kutoka 15 mwaka 2006 hadi kufikia changamoto 3 kwaka huu 2017, Muungano unaotimiza miaka 53 wiki ijayo.

Waziri Makamba amezungumza hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa katika mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na waratibu wa  sherehe za kitaifa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Walemavu na kusimamiwa na Waziri Mwenye dhamana Mhe Jenista Mhagama.

Mhe. Makamba amezitaja changamoto zilizobakia kuwa ni pamoja na usajili wa vyombo vya moto unaorahisisha kusafirisha magari kutoka Zanzibar kwenda Bara na  kutoka Bara kwenda Zanzibar na kusema kuwa swala hili linafanyiwa kazi kwa kumalizwa  kwa taratibu za kisheria.

Alisema kuwa changamoto nyingine inahusu Hisa za Zanzibar kwa iliyokuwa bodi ya safari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Pamoja na Mapendekezo ya tume ya Pamoja ya fedha.

Awali akizungumzia Muungano huo unaotimiza miaka 53, Waziri Makamba Alisema kuwa  umekuwepo kisheria na  umerasimisha  udugu na ushirikiano uliyokuwepo kati ya Bara na Visiwani.

Mkutano huo wa waandishi wa habari uliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Walemavu umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Jordan Rugimbana, Makatibu Wakuu na Wakurugenzi wa Ofisi hizo.

No comments:

Post a Comment