NA SELINA WILSON, TARIME
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John
Magufuli, amesema watumishi wa serikali
watakaoboronga kazi hawatahamishwa vituo vya kazi, badala yake watatimuliwa
mara moja.
Amesema kumekuwa na mtindo wa watendaji wa serikali
kufanya kazi na kuharibu kisha kuhamishiwa vituo vingine, lakini katika serikali
atakayoiongoza atahakikisha mtumishi anayeharibu kazi anaondolewa moja kwa moja.
Dk. Magufuli alisema hayo jana alipozungumza kwa nyakati
tofauti na wakazi wa Nyamongo, Tarime, Rorya na Musoma katika mikutano ya
kampeni za uchaguzi mkuu zinazoendelea mkoani Mara.
Alisema akipata ridhaa ya wananchi akiwa Rais, anataka
watendaji wa serikali wachape kazi na kwamba, atakayeharibu kazi ajue ameharibu
maisha yake kwa kuwa hatapata nafasi ya kwenda kuharibu mahali pengine.
“Mtendaji akiharibu kazi ajue anakwenda nyumbani moja kwa
moja. Serikali ya Magufuli kutakuwa hakuna mambo ya hamahama. Nataka watu
wafanye kazi,” alisema na kuongeza kuwa wananchi wamekuwa wakiichukia serikali
kwa sababu ya watendaji wachache wanaoshindwa kutekeleza majukumu na kuwasababishia
kero.
Dk. Magufuli aliwataka wananchi wamuunge mkono katika
msimamo wake wa kutohamisha watendaji wa serikali wanaoharibu kazi kwa kusema
‘hakuna kuhama’ kwa kuwa watendaji hao ndio wamekuwa kikwazo cha maendeleo ya
watu.
Akiwa Rorya Dk. Magufuli aliwataka wananchi kuacha uvuvi
wa kutumia mabomu kwa kuwa rasilimali zilizomo ziwani zinapaswa kutunzwa ili zitumike
kwa maendeleo ya wananchi wote.
“Mkitumia sumu kuvua mnaua mpaka mayai ya samaki. Hivi
mayai yakikosekana watoto watazaliwa.. Serikali ya awamu ya tano itatoa mikopo
kwa wavuvi na kushusha bei ya vifaa vya uvuvi ili wananchi wapate urahisi
kwenye shghuli zao,”alisema.
Kwa upande wake, Mgombea ubunge wa jimbo la Bunda,
Stephen Wassira akizungumza Mjini Tarime alisema wananchi wanapaswa kujenga
amani na umoja kwa kutokubali kupotoshwa na watu wanaosema watawaletea
mabadiliko ambayo hawawezi kuyatekeleza na kwamba Dk. Magufuli ndiye chaguo
sahihi kwa maendeleo yao.
Awali, Dk. Magufuli aliwatumia salamu wawekezaji kufanya
shughuli zao kwa kufuata sheria na kuweka uwazi kwenye hesabu za mapato
yatokanayo na uchimbaji wa madini.
Hatua hiyo itawezesha wawezekezaji kulipa kodi stahiki,
ajira na kutoa huduma kwa wananchi wanaozunguka migodi kwa kuleta
maendeleo katika maeneo hayo.
Mgombea huyo alisema hayo alipozungumza na wakazi wa Nyamongo wilayani Tarime ambako kuna mgodi
wa North Mara.
“Ukimpa mtu biashara yako lazima atoe hesabu ijulikane
faida ni ipi na kama kuna hasara pia ijulikane. Kwenye serikali yangu nitalisimamia
hili ili wananchi na serikali ipate manufaa ya uwekezaji.
Wawekezaji tunawapenda, lakini tunataka biashara pasu kwa
pasu. Tunataka tujue mapato ya uwekezaji sio waje wachote madini watuachie
mashimo,” alisema.
Alisema hatakubali wananchi wanyonywe bila kunufaika na
uwekezaji kwenye migodi ambayo wawekezaji wachimba wanaacha mashimo.
“Mimi sichukii migodi, nataka wawekezaji waje wengi
lakini na wananchi wanufaike. Najua kuna malalamiko mengi kuna watu
wamechukuliwa maeneo yao na nataka mlipwe fedha zenu,”alisema.
Dk. Magufuli alisema anashangazwa kusikia Nyamongo kuna
tatizo la maji na kusema kwamba hakuna sababu ya kukosa maji wakati kuna mgodi
na wawekezaji wanazalisha hivyo wanapaswa kutoa huduma hiyo kwa wananchi.
Kwa upande wa wachimbaji wadogo, alisema serikali
itaendelea kuwawezesha kupata mitaji kwa kuwapa mikopo ya fedha na vifaa ili
wafanye kazi zao kwa ufanisi, suala ambalo limekwishaanzishwa na serikali
iliyopo.
Katika hatua nyingine, aliwaomba wazee wa koo na viongozi
wilayani Rorya na maeneo mengine wakae chini kuzungumzia namna ya kudhibiti
wizi wa ng’ombe ambao umekuwa kero kwa wananchi na kutishia kukwamisha maendeleo
ya watu.
Hata hivyo aliwaahidi kuwa akiingia Ikulu atatumia polisi
na mitambo ya kamera (CCTV) kudhibiti wizi huo.
“Zipo kamera zinaweza kufungwa na kuona kilometa 15 hadi
30, tutawapatia askari polisi ili wazitumie kudhibiti wimbi la wizi wa n g’ombe.
Inauma mno unaamka asubuhi unakuta zizi liko wazi, ulikuwa unategemea maziwa
yanakuwa hakuna,”alisema.
Kutoka
Itilima mkoani Simiyu Chibura Makorongo anaripoti kuwa, Mjumbe wa Timu ya
Ushindi ya CCM, Mwigulu
Nchemba, amezindua kampeni za Chama wilayani humo na kuwaomba wananchi wampe
kura nyingi Dk. Magufuli.
Nchemba
alisema Dk. Magufuli ndiye jibu sahihi la utatuzi wa kero za wananchi kwa kuwa
ana rekodi nzuri ya utendaji wa kazi nchini.
Mwigulu
alisema kuwa Tanzania inakabiliwa na matatizo matatu ambayo aliyataja kuwa ni
watu waliosoma kwa kodi za Watanzania na wakaaminiwa na kupewa dhamana, lakini
wanafanya kazi kizembe, ukosefu wa uaminifu na utapeli miongoni mwa watu
walioaminiwa.
Alisema
mgombea huyo ni kiboko cha matapeli na mafisadi, na pia wanaofanya kazi kizembe
na kwamba iwapo Watanzania watamchagua atawashughulikia ikiwa na pamoja na
kuhakikisha taifa linasonga mbele.
“Magufuli
hana rafiki kwenye utendaji. Tangu ujana wake rafiki yake ni Tanzania na kazi
anayopewa kuisimamia tu basi leo hii tunaona baadhi ya wagombea wanafadhiliwa
na mafisadi wote na tutakapowapa nchi lazima waibe kwanza walizotumia kwenye
kampeni tusiwakubali katisa kuwachagua,”aliongeza.
Aidha
Mwigulu aliwabeza wagombea wengine wa nafasi ya urais na hasa mgombea urais kwa
tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chini ya mwamvuli wa
UKAWA, Edward Lowassa na kusema kuwa ni msanii wa kutafuta madaraka na hana nia
njema na nchi.
“Lowassa
kwa miaka 40 mimi nazaliwa anatembelea gari ila leo wakati wa kutafuta urais
ndio anapanda daladala? Lowassa ni maarufu tangu akiwa na umri wa miaka 40 na
angeweza kuwa rais kama sio rekodi yake ya kutiliwa mashaka tangu wakati wa Hayati
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere,”alisema Mwigulu.
“Lowasa
anatiliwa mashaka kwa sababu wakati wote amezungukwa na wapiga dili na hata
chama alichokwenda amepokelewa kwa dili. Msipotoshwe na wapiga dili maana
kinachowasukuma sio matatizo ya Watanzania bali ni kutaka kurudisha pesa
walizotumia tangu mchakato wa kuteua mgombea ndani ya chama,” alisema mjumbe
huyo.
No comments:
Post a Comment