Thursday, 17 September 2015

DK MAGUFULI APOKEWA KIFALME KIGOMA

Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli akiwahutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kawawa
Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli akiwahutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Kawawa
Maelfu ya wananchi waliofurika kwenye uwanja wa Kawawa wakimsikiliza Dk. Magufuli
Dk. Magufuli akinadi sera na ilani ya CCM
Nyomi si la kawaida
NA CHARLES MGANGA, GEITA

MGOMBEA urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, ameendelea kuwasisitiza wananchi wa mikoa ya Kigoma na Kagera kulinda amani iliyopo nchini.

Katika mikutano yake ya kampeni juzi, Dk. Magufuli alisema amani iliyopo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote, kwani ikitoweka ni kazi kuipata.

Alisema akichaguliwa kuwa rais, atahakikisha anailinda amani kwa namna yoyote ili wananchi waendelee kuishi vizuri na kufanya kazi zao bila hofu yoyote.

Aliongeza kuwa ni vyema kila mwananchi akawa mlinzi wa mwenzake ili kuweza kuwadhibiti raia wasio na nia njema na Tanzania.

Dk. Magufuli alisema hakuna sababu kwa askari kuendelea na utaratibu wa kuyasindikiza mabasi katika mikoa hiyo, kwa sababu ya kulinda raia wa mali zao mikoa hiyo ya mipakani.

“Askari wamekuwa wakisindikiza mabasi katika maeneo hatarishi katika mipaka ya mikoa hiyo.

“Nadhani ufike wakati sasa, askari waendelee na majukumu mengine na siyo, kusindikiza mabasi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema raia wa nchi jirani wenye nia mbaya, hawana nafasi nchini na wanapaswa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.

“Sisi ndiyo tunaowakaribisha wenzetu kutoka nje ya nchi, kama tutafanya utaratibu wa kutoa taarifa kwa wale tunaodhani wana mashaka na usalama wetu, tutoe taarifa haraka,” alisema katika maeneo yote aliyopita.

Kwa kuonyesha ni suala nyeti, Dk. Magufuli alisema watakaoichezea amani, atahakikisha anawashughulikia ipasavyo.

Alisema wakimbizi wakija nchini, wanapaswa kuacha mabomu yao kwani Tanzania ni kisiwa cha amani katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Kwa kweli atakayeichezea amani nchini, nitahakikisha nitalala naye mbele. Amani tunapaswa kuilinda kwa nguvu zote, atakayeichezea tupambane nae,” alisisitiza.

Alisema ni kosa kwa wananchi wa Kagera na Kigoma, kushirikiana na watu wabaya wanaoingia nchini na kuwa wakimbizi hao, wanaoingia nchini wanapaswa kuilinda amani watakayoikuta.

Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unatarajiwa kufanyika nchini kote Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment