Saturday, 19 September 2015

MAGUFULI ALIPOHUTUBIA MKUTANO WA KAMPENI BUHIGWE, AWATAKA WANANCHI KULINDA AMANI ILIYOPO

NA CHARLES MGANGA, GEITA

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, ameendelea kuwasisitiza wananchi wa mikoa ya Kigoma na Kagera kulinda amani iliyopo nchini.

Katika mikutano yake ya kampeni juzi, Dk. Magufuli alisema amani iliyopo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote, kwani ikitoweka ni kazi kuipata.

Alisema akichaguliwa kuwa rais, atahakikisha anailinda amani kwa namna yoyote ili wananchi waendelee kuishi vizuri na kufanya kazi zao bila hofu yoyote.

Alisema ni vyema kila mwananchi akawa mlinzi wa mwenzake, ili kuweza kuwadhibiti raia wasio na nia njema na Tanzania.

Dk. Magufuli alisema hakuna sababu kwa askari kuendelea na utaratibu wa kuyasindikiza mabasi katika mikoa hiyo, kwa sababu ya kulinda raia wa mali zao mikoa hiyo ya mipakani.

“Askari wamekuwa wakisindikiza mabasi katika maeneo hatarishi katika mipaka ya mikoa hiyo.

“ Nadhani ufike wakati sasa, askari waendelee na majukumu mengine na siyo, kusindikiza mabasi,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema raia wa nchi jirani wenye nia mbaya, hawana nafasi nchini na wanapaswa wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.

“Sisi ndiyo tunaowakaribisha wenzetu kutoka nje ya nchi, kama tutafanya utaratibu wa kutoa taarifa kwa wale tunaodhani wana mashaka na usalama wetu, tutoe taarifa haraka,” alisema mgombea huyo katika maeneo yote aliyopita tangu juzi.

Kwa kuonyesha ni suala nyeti, Dk. Magufuli alisema watakaoichezea amani, atahakikisha anamshughulikia ipasavyo.

Alisema wakimbizi wakija nchini, wanapaswa kuacha mabomu yao kwani Tanzania ni kisiwa cha amani katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Kwa kweli atakayeichezea amani nchini, nitahakikisha nitalala naye mbele. Amani tunapaswa kuilinda kwa nguvu zote, atakayeichezea tupambane nae,” alisisitiza.

Alisema ni kosa kwa wananchi wa Kagera na Kigoma, kutoshirikiana na watu wabaya wanaoingia nchini.

Alisema wakimbizi hao, wanaoingia nchini, wanapaswa kuilinda amani watakayoikuta.

Uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unatarajiwa kufanyika nchini kote Oktoba 25, mwaka huu.

Wakati huo huo, mgombea urais wa CCM, John Magufuli amesema ameamua kufanya kampeni kwa kusafiri maeneo yote nchini kwa kutumia usafiri wa barabara, ili naye ajionee adha wanayopata wananchi.

Akizungumza katika kampeni zake mjini Kibondo, mkoani Kigoma, Dk. Magufuli, alisema hakutaka kutumia helkopta au ndege kama wanavyofanya wagombea wengine.
Alisema kufanya hivyo, ni kushindwa kuyafahamu matatizo ya wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

“Nimeamua kutumia usafiri wa gari kote niendako ili name niumie mgongo, niyapate maumivu mnayopata ninyi mnaposafiri. Nitakapokuwa Ikulu nijue kwamba mnakabiliana na changamoto ambayo naifahamu kwa kiasi kikubwa,” alisema mgombea huyo.

Hata hivyo, Dk. Magufuli alisema serikali ya awamu ya nne, imefanya makubwa katika sekta ya ujenzi wa barabara nchini tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alipokuwa katika uwanja wa Simpombe, jimbo la Kigoma Kusini, Dk. Magufuli alisema hali ya barabara katika eneo la Nguruka haikuwa hivyo miaka ya zamani.

Alisema zamani barabara ya Nguruka haikuwepo, lakini hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.

“Jamani zamani usafiri wa uhakika ulikuwa ni treni peke yake, ukiikosa umekwisha. Waziri nitakayemteua kuongoza Wizara ya Ujenzi, nataka afanye kazi kwelikweli,” alisema.

Aliwaahidi wakazi wa Nguruka kujenga barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita tatu.

“Nikisema huwa nimesema. Niliwaambia tutajenga daraja pale Maragarasi, tumeifanya hivyo na Rais Jakaya Kikwete ameshafungua daraja hilo,” alisema Dk Magufuli.

Maeneo mengine ambayo Dk. Magufuli ameahidi ujenzi wa barabara ni ukamilishwaji wa barabara ya Kigoma- Urambo, ambayo hupita Nguruka, Mwandiga hadi Manyavu nayo itajengwa kwa kiwango cha lami.

Pia, Dk. Magufuli alisema barabara ya Manyovu - Kasulu mpaka Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 48, itajengwa na kutoa ahadi nyingine ya kilomita tano katika mji wa Kasulu.

Dk. Magufuli alisema mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kasulu – Kibondo, amepatikana na baada ya taratibu za kawaida kukamilika, ataanza kazi wakati wowote.

Alisema amewahakikishia wakazi wa wilaya mpya ya Kakonko, kwamba mkandarasi atakapomaliza kazi ya ujenzi, majengo yatatumika kwa mahitaji ya maendeleo ya eneo hilo.

“Nimepokea ombi kwamba mnataka majengo myatumie baada mkandarasi kumaliza kazi. Hilo halina shida, nitawapa muamue wenyewe kama mnataka kufanya chuo cha ufundi au vipi, mtajua wenyewe,” alisema Dk. Magufuli.

Aliwapongeza wananchi wa Kakonko kwa eneo lao kuwa wilaya mpya, hivyo anaamini kasi ya maendeleo itaongezeka kwani fedha zinazotolewa, zinafanyia kazi ipasavyo.

No comments:

Post a Comment