Sunday, 27 September 2015

DK. MAGUFULI AWASHTUKIA WASALITI CCM


Na Chibura Makorongo, Shinyanga

MGOMBEA urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli amerudia kauli yake ya kuwakemea baadhi ya wana CCM ambao mchana huimba ‘iyena iyena’ wakiiunga mkono CCM, lakini unapoingia usiku hukimbilia kwenye vyama vya upinzani.

Aliwataka wanachama hao kuacha mara moja tabia hiyo vinginevyo atalazimika kuwataja hadharani na kuwaumbua.

Hata hivyo, alimtaja mmoja wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mkoani Shinyanga kuwa ni mmoja wa watu hao.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akihutubia maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga na kukemea vitendo vya baadhi ya wana CCM aliodai ni wanafiki.

Alieleza kusikitishwa kwake na wana CCM hao wanaoonyesha usaliti na unafiki wa wazi ambapo alisema ni vizuri wakawafuata wanafiki wenzao walioamua kumfuata aliyekuwa Waziri Mkuu aliyeondoka madarakani kwa kashfa, Edward Lowassa na kwamba hakosei pale anapowaita wanafiki.

“Wabaya hawako kwenye vyama vingine tu, hata humu ndani ya CCM wamo, kwani Mgeja (Khamis) hakuwa CCM?  Hawa wanaogombea huko kwingine hawakuwa CCM, waliohama hawaitukani CCM leo hii…kwa nini hawakutukana walipokuwa CCM.  Je, tukiwaita wanafiki tunakosea?” alihoji.

“Hapa Shinyanga wapo watu ambao asubuhi wanasema Masele oyeee, Magufuli oyeee, lakini usiku ukiingia wako kwingine na bahati nzuri wengine nawafahamu mpaka majina yao, kuna mtu anaitwa Gaspar, ni mfanyabiashara," alisema Dk. Magufuli.

Aliongeza kuwa: "Mimi daima nasema ukweli sifichi kitu, nasikia huyu bwana mchana yupo CCM usiku yuko kwingine, ndiyo tatizo la wana wa Shinyanga, saa nyingine tunatumiwa, tunachezewa,” alieleza Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli alisema ili CCM iweze kupata ushindi wa kishindo ni lazima wana CCM wenyewe waonyeshe mshikamano wa dhati katika kipindi chote cha kampeni na siku ya kupiga kura wamchague yeye awe rais wa awamu ya tano na wabunge na madiwani wanaotokana na CCM.

Dk. Magufuli alisema iwapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania atahakikisha anatekeleza kwa vitendo ahadi zake anazozitoa bila kubagua watu kwa misingi ya vyama vyao vya siasa na kila siku hulala akimuomba Mwenyezi Mungu ili amsaidie asisahau ahadi hizo wakati wa kuzitekeleza.

“Tunataka Tanzania iwe ni nchi yenye maendeleo makubwa, serikali ijayo ya awamu ya tano chini ya Magufuli itakuwa ni ya vitendo na ya kazi, ndiyo maana kila siku nasema hapa ni kazi tu. Naomba mnipe urais jamani niwatumikie,  Tanzania itakuwa ni ya viwanda, sintowaangusha,”Dk. Magufuli aliwaomba wananchi hao.

“Kwa hapa Shinyanga ninajua kuna changamoto nyingi na kuna kero ya kutokuanza kazi kwa kiwanda chenu cha nyama, lakini nataka niwahakikishie, nikiwa rais wa nchi hii, kiwanda hiki kilichokwama kufanya kazi miaka mingi kitaanza kazi, nasema lazima kianze uzalishaji,” alisisitiza.

“Ninaomba nimuagize mmiliki wake ahakikishe pale atakaposikia nimeapishwa rasmi kuwa Rais wa Tanzania na yeye huku ahakikishe kiwanda hicho kinaanza kufanya kazi, vinginevyo yeye mwenyewe akirejeshe serikalini, tutakiendesha wenyewe,” alieleza Dk. Magufuli.

Kuhusu suala la miundombinu ya barabara, Magufuli  alisema serikali yake itaendelea kuboresha barabara zote nchini kwa kuzijenga kwa kiwango cha lami na kuboresha reli ya kati ambayo tayari maandalizi ya ujenzi wake yameanza ili kuboresha huduma ya usafiri katika mikoa ya kanda ya kati na ziwa.

Aliwataka wakazi wa Mkoa wa Shinyanga waendelee kuwa na imani na CCM ambacho ndicho pekee chenye uwezo wa kuwaletea mabadiliko ya kweli.

Kwa upande mwingine, amewaomba wakazi wa Shinyanga mjini kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Stephen Masele, ambaye kwa kipindi kifupi tangu alipochaguliwa mwaka 2010 ameonyesha ufanisi katika utendaji wake wa kazi na kwamba hata kama ana mapungufu basi ni yale ya kibinadamu.

“Ninawaomba sana watu wa Shinyanga, kwanza tumtangulize Mungu mbele wakati wa kupiga kura, naomba msinichanganyie watu, ukipenda kufuli, basi penda na funguo zake tatu ili iwe rahisi kulifungua hilo kufuli, ndiyo maana tunasema ukinichagua mimi, mchagueni Masele na madiwani wa CCM,” alieleza Dk. Magufuli.

Awali, akihutubia mkutano mwingine wa kampeni uliofanyika kwenye jimbo la Solwa, mjumbe wa timu ya kampeni za CCM, Samuel Sitta alimpongeza mgombea ubunge wa jimbo hilo, Ahmed Salum kwa jinsi alivyotekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 – 2015 katika jimbo lake.

Sitta alisema Salum ni miongoni mwa wabunge wachapa kazi ndani ya CCM na kuwaomba wananchi wa Jimbo la Solwa wasimpoteze na wahakikishe wanampigia kura nyingi za kishindo ili aweze kukamilisha miradi mingi ya maendeleo aliyokwisha ianzisha kwenye jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment