Sunday, 27 September 2015

SAMIA: WAZEE MSIWE NA HOFU


NA KHADIJA MUSSA, MIKUMI

MGOMBEA Mwenza wa urais kupitia CCM, Samia Suluhu Hassan, amewataka wazee kutokuwa na wasiwasi wa kupata huduma kwa sababu Chama kimeweka mikakati kabambe ya kuboresha maisha yao.

Amesema katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuna mikakati mbalimbali imewekwa kwa ajili ya kuboresha huduma za wazee.

Samia alisema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye jimbo la Mikumi mkoani Morogoro.

Alisema wakifanikiwa kuingia madarakani watafanya uhakiki wa wazee nchi nzima ili waweze kupata idadi kamili kwa ajili ya kuwapatia mafao.

Mgombea mwenza huyo alisema serikali inatambua kuwa wazee wengi wamekuwa wakiishi kwa tabu kutokana na kutopewa kipaumbele cha kutosha jambo ambalo awamu ya tano imepanga kulirekebisha.

Samia alisema serikali ijayo imeamua kutoa kipaumbele kwa wazee ili nao waweze kunufaika na taifa lao, hivyo aliwaomba kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na kumchagua Dk. John Magufuli ili aweze kuwa rais.

Akizungumzia kuhusu kuvamiwa na wanyama kwa wakazi wa eneo hilo, Samia alisema suala hilo watalifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya uhifadhi na wanyamapori.

Kwa mujibu wa Samia, anafahamu ukubwa wa tatizo hilo na kwamba watahakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuwaondolea adha hiyo ya wao na mashamba yao kuvamiwa na wanyama.

No comments:

Post a Comment