NA HAPPINESS MTWEVE, Dodoma
MGOMBEA ubunge jimbo la Dodoma Mjini
kwa tiketi ya CHADEMA, Benson Kigaila, leo anatarajiwa kufikishwa kwenye
Mahakama ya Wilaya mkoani hapa, kujibu mashitaka ya kumpiga askari polisi na
kumjeruhi kwa chupa pamoja na kufanya fujo katika kituo cha kati cha polisi.
Mashitaka mengine yanayomkabili
Kigaila, ambaye ni Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, ni
kukiuka amri halali ya polisi na kufanya maandamano bila kibali.
Mbali na Kigaila, wapo wanachama
wengine 10 wa chama hicho ambao wote kwa pamoja wanashikiliwa kwa tuhuma hizo
na watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Dodoma, David Misime, watuhumiwa
wengine ni Mwenyekiti wa Vijana wa CHADEMA mkoa wa Dodoma, Godfrey Manyanya
(29), Hashim Kilaini (45), Alex Thomas(28), Khadija Maula (40) na Stellah
Massawe (38).
Wengine ni Prisca Mgaza (20),
Luckyson Kweka (28), Aisha Urio (22), Pompey Remijo (40) na Lawi Tumuza (52).
Akielezea tukio hilo, Kamanda Misime
alisema watuhumiwa hao walifanya makosa hayo juzi, saa 12:45 jioni wakiwa
kwenye barabara ya Jamatini.
Alisema wafuasi hao walifanya maandamano bila kibali na kuzuia watumiaji wengine wa barabara kuendelea na shughuli zao licha ya kupewa maelekezo ya askari kuwataka kutokufanya hivyo.
Watuhumiwa hao kwa pamoja walikaidi
maagizo hayo ya polisi na kuanza kutoa lugha za matusi na kumshambulia na
kumjeruhi askari kwa chupa ya soda.
Askari aliyejeruhiwa aliyetambulika
kwa jina la PC Rebecca, alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa kwa
matibabu.
Kamanda Misime alitoa wito kwa
wagombea wa vyama vyote vya siasa na wananchi wa Dodoma, kutii sheria bila
shuruti kwani umaarufu hautafutwi kwa kuvunja sheria na watambue kufanya hivyo
ni kosa la jinai.
Aliwataka wanasiasa watambue kuwa
hakuna haki isiyokuwa na wajibu, hivyo wanatakiwa kutimiza wajibu wao kwa
kuhakikisha wanapokwenda na kutoka kwenye mikutano, hawafanyi maandamano.
Alisema hata watunapotumia barabara,
wanapaswa kuzingitia sheria za usalama barabarani, ili watu wengine waendelee
na shughuli zao bila kubughudhiwa wala kutishwa.
No comments:
Post a Comment