Sunday, 27 September 2015

MAGUFULI; NITAWABEBA WACHIMBAJI WADOGO





NA CHARLES MGANGA, BUKOMBE

MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, ameahidi serikali yake haitakubali wachimbaji wadogo wadogo kunyanyaswa kwa kunyang'anywa maeneo yao.


Magufuli amesema watu wachache wenye tabia ya kuwaonea wa wachimbaji hao, hawatavumiliwa.
 
"Sitakubali wachimbaji wadogo kuchukuliwa maeneo yao  baada ya kuyagundua," alisema.


Dk. Magufuli, ambaye alipokewa kwa idadi kubwa ya wakazi wa Bukombe, alisema serikali yake itakachofanya ni kuhakikisha maeneo ya wachimbaji wanapewa wahusika hao.


Kwa majibu wa Ilani ya Uchaguzi mkuu ya mwaka 2015, Dk. Magufuli alisema wachimbaji watawezeshwa kwa kapewa mikopo ili waweze kufanyakazi zao kwa ufanisi.
 
Pia, wachimbaji hao watapewa vifaa bora kwa ajili ya uchimbaji madini na kuwawezesha kupata leseni za uchimbaji.


"Wale wanaodhulumu wachimbaji madini sitawavumilia, tutawawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kunufaika na rasilimali za nchi yao," alisema mgombea huyo wa CCM.


Dk. Magufuli, ambaye alikuwa njiani akitokea Kagera kwenda Geita, alisema maeneo ya uchimbaji dhahabu yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo.

Alisema ameomba nafasi ya urais ili pamoja na mambo mengine, atatue changamoto za wachimbaji wa madini.


Ili kuthibitisha serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuwapa maisha bora wachimbaji, Dk. magufuli alimuita mgombea ubunge Jimbo la Shinyanga Mjini, Steven Masele kufafanua kilichomo kwenye Ilani ya Uchaguzi.


Masele, ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alisema tayari maeneo kwa ajili ya uchimbaji madini yametengwa.
 
Alisema kuna maeneo yametengwa Pori la Runzewe lililopo Turawaka na kuahidi watanufaika nalo kwa majibu wa ilani.

No comments:

Post a Comment