Saturday, 12 September 2015

LUSINDE; LOWASSA MUONGO MPUUZENI




NA ABDALLAH MWERI, BAGAMOYO

MWANASIASA machachari na Mbunge wa Jimbo la Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, amewataka wananchi kupuuza kauli ya Mgombea wa Urais kupitia CHADEMA, Edward Lowassa kuwa akiingia madarakani ataboresha wodi za wanawake nchini.

Lusinde alitoa kauli hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika juzi Bagamoyo, Pwani na Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan.

Bendera ya CCM katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu inapeperushwa na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli.

Lusinde amewataka wananchi kumpuuza, Lowassa kwa kuwa kauli zake za kuboresha wodi za kina mama wanaojifungua zina lengo la kuwahadaa wapiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.

"Ndugu zangu asije mtu akadai eti ana uchungu na wananchi ataboresha wodi za kina mama, huu ni uongo mkubwa Lowassa na Sumaye waache kutoa kauli za kupotosha mbona hawakufanya hivyo walipokuwa mawaziri wakuu,"alisema Lusinde.

Alisema Lowassa na Sumaye hawana uchungu mkubwa kuhusu changamoto zinazowapata kina mama kama Samia ambaye ni mama wa watoto wanne.

"Hivi hawa watu wanavyodai wana uchungu kuona vifo vya kina mama wanaojifungua, naomba muwaulize kwani walishawahi kuingia leba kama ilivyo kwa Samia ambaye ni mama mwenye watoto," alisema Lusinde.

Mbunge huyo aliyekuwa akishangiliwa kwa nguvu katika mkutano huo, alisema Lowassa na Sumaye hawana jipya na amewataka kusahau kuingia Ikulu katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Lusinde aliwataka wakazi wa Bagamoyo mkoani Pwani kumpigia kura za ushindi Dk. Magufuli ili afanye kazi na Samia katika serikali ya awamu ya tano.

Mbunge huyo aliwataka wananchi kuichagua CCM kwa kuwa ndio chama pekee kinachotekeleza ilani na kimeleta maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali.

No comments:

Post a Comment