NA CHARLES MGANGA, GEITA
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema anafanya
kampeni kwa usafiri wa barabara kwenye maeneo yote nchini ili aendelee kufahamu
matatizo ya Watanzania.
Akizungumza katika kampeni zake mjini Kibondo, mkoani
Kigoma, Dk. Magufuli, alisema hakutaka kutumia helkopta au ndege kama
wanavyofanya wagombea wengine.
Alisema kufanya hivyo ni kushindwa kuyafahamu
matatizo ya wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.
“Nimeamua kutumia usafiri wa gari kote niendako ili
niumie mgongo, niyapate maumivu mnayopata ninyi mnaposafiri. Nitakapokuwa Ikulu
nifahamu kwamba mnakabiliana na changamoto ambayo naifahamu kwa kiasi kikubwa,”
alisema.
Hata hivyo, Dk. Magufuli alisema serikali ya awamu ya
nne, imefanya makubwa katika sekta ya ujenzi wa barabara nchini tofauti na hali
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alipokuwa katika Uwanja wa Simpombe, jimbo la Kigoma
Kusini, Dk. Magufuli alisema hali ya barabara katika eneo la Nguruka haikuwa
hivyo miaka iliyopita.
Alisema zamani barabara ya Nguruka haikuwepo, lakini
hali imebadilika kwa kiasi kikubwa.
“Jamani zamani usafiri wa uhakika ulikuwa ni treni
peke yake, ukiikosa umekwisha. Waziri nitakayemteua kuongoza Wizara ya Ujenzi,
nataka afanye kazi kwelikweli,” alisema.
Aliwaahidi wakazi wa Nguruka kujenga barabara kwa
kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita tatu.
“Nikisema huwa nimesema. Niliwaambia tutajenga daraja
pale Malagarasi, tumeifanya hivyo na Rais Jakaya Kikwete ameshafungua daraja
hilo,” alisema Dk. Magufuli.
Maeneo mengine ambayo Dk. Magufuli ameahidi ujenzi wa
barabara ni ukamilishwaji wa barabara ya Kigoma- Urambo, ambayo hupita Nguruka,
Mwandiga hadi Manyovu nayo itajengwa kwa kiwango cha lami.
Pia, Dk. Magufuli alisema barabara ya Manyovu -
Kasulu mpaka Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 48, itajengwa na kutoa ahadi
nyingine ya kilomita tano katika mji wa Kasulu.
Alisema mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya
Kasulu – Kibondo, amepatikana na baada ya taratibu za kawaida kukamilika,
ataanza kazi wakati wowote.
Alisema amewahakikishia wakazi wa wilaya mpya ya
Kakonko kwamba mkandarasi atakapomaliza kazi ya ujenzi, majengo yatatumika kwa
mahitaji ya maendeleo ya eneo hilo.
“Nimepokea ombi kwamba mnataka majengo myatumie baada
mkandarasi kumaliza kazi. Hilo halina shida, nitawapa muamue wenyewe kama
mnataka kufanya chuo cha ufundi au vipi, mtajua wenyewe,” alisema Dk. Magufuli.
No comments:
Post a Comment