Na Waandishi Wetu
NI dhahiri kundi la UKAWA na mgombea urais wao,
Edward Lowassa, wameshikwa pabaya na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli,
ambapo sasa wameanza kuweweseka.
Dk. Magufuli, ambaye amekuwa akipata umati mkubwa
kwenye mikutano yake ya kampeni na maeneo yote anayopita, amekuwa mahiri katika
kunadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kutoa ahadi zinazotelekezeka.
Pia, timu ya makada wa CCM ambayo imekuwa ikizunguka
naye kwenye maeneo mbalimbali nchini, imekuwa kikwazo kikubwa kwa UKAWA na
mgombea wao, ambaye amekuwa akishindwa kunadi Ilani na kuzungumza kwa dakika
chache.
Hilo limekuwa kikwazo kikubwa na sasa UKAWA wameibuka
na madai mapya wakidai CCM kinavunja
kanuni na taratibu za uchaguzi, jambo ambalo hawatakubaliana nalo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, jana, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alidai kauli zinazotolewa
na makada wa CCM akiwemo Mwenyekiti wa WAZAZI Taifa, Abdlaah Bulembo,
zinaashiria vurugu.
Kwa mujibu wa Mbowe, Bulembo alikaririwa akizungumza kwenye
mikutano ya kampeni akisema kuwa CCM haitakuwa tayari kuachia Ikulu.
Mbowe alisema kauli hiyo ni ya uchochezi na inaondoa
umuhimu wa uchaguzi kwa kuwa tayari CCM imeshafanya uamuzi na kwamba, Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijakemea mpaka sasa.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Shaka Hamdu
Shaka, amesema kauli ya Mbowe ni ishara kuwa wameshikwa pabaya na mgombea wao
hana uwezo wa kupambana na Dk. Magufuli.
Alisema CHADEMA ni mabingwa wa siasa chafu kwani,
juzi walitangaza kumfikisha Dk. Magufuli mahakamani na sasa wamemgeukia
Bulembo, lakini watambue kipigo kiko pale pale.
Katika mkutano huo, Mbowe mbali na kuibua madai hayo
pia alikiri UKAWA kukabiliwa na changamoto nzito ya mgawanyo wa majimbo.
Alisema shutuma zinazotolewa na viongozi wa vyama
vingine vinavyounda UKAWA dhidi ya CHADEMA, hazina tija na kuwa ukweli
wanaujua.
Alisema shutuma hizo zinaonyesha kuwa viongozi hao
wamefika thamani ya bei na hawatambui kuwa vyama na wagombea wao hawana uwezo
wa kuongoza.
Alisema viongozi hao kamwe wasitarajie CHADEMA kuwapa
majimbo ya uchaguzi kama zawadi na badala yake vigezo huangaliwa.
Alhamisi Makamu Mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI, Leticia
Masore, Katibu Mkuu Mosena Nyambabe na viongozi wengine wa juu, walilalamikia
hatua ya CHADEMA kuwaburuza na kumtaka Mwenyekiti wao, James Mbatia, kutetea
maslahi ya chama.
Pia, wameahidi kupambana kuhakikisha hadhi na heshima
ya chama hicho inarejea tofauti na ilivyo sasa ambapo, kimedhoofika baada ya
kujiunga na UKAWA.
“Watu wanalalamika wakati wanajua vyama vyao na
wagombea hawana uwezo wa kuongoza… kupata jimbo ni kazi nzito sio wanalialia tu
ooh tumenyimwa majimbo kwani hawajui hawana sifa za kugombea na kushinda.
“Nawashauri waache kupiga kelele na kumshambulia Mbatia…wakajipange
kisiasa.
Wanalalamika wajue wamenyimwa majimbo likiwemo la
Serengeti na Segerea ambapo, jimbo mojawapo tumempa Julius Mtatiro…mgombea wetu
ana sifa zote za kushinda, lakini CUF walituomba tukamuachia na tukisema
aendelee na kampeni peke yake bila kumuunga mkono hatashinda, hivyo wasitegemee
walale wapewe viti,” alisema Mbowe.
Aliwaponda viongozi hao kuwa kelele zao ni mwendelezo
wa siasa za majitaka ambazo zimewahi kufanywa na baadhi ya viongozi wengine wa
UKAWA akiwemo Dk. Wilibroad Slaa.
Aidha, Mbowe alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa
Mbatia ana ulinzi wa kutosha wa vijana wa Red Bridged, kauli ambayo inaashiria
kuwa ndani ya NCCR-Mageuzi hali ni mbaya.
Hata hivyo, alikiri changamoto kwenye mgawanyo wa majimbo
ni kubwa na kwamba, wataendelea kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake, Shaka alisema madai ya Mbowe hayana
tija kwani wao ndio wamekuwa vinara wa kutoa kauli za kuvuruga amani.
Alisema matamshi yanayotolewa na viongozi wa UKAWA ni
hatari ikiwemo kuwataka wananchi kutoondoka vituoni ili kulinda kura, kufanya
kampeni kwa misingi ya udini, kuandaa vijana kwa ajili ya vurugu na kutangaza
kuwa wataibiwa kura.
“Hizi ni kauli za mfa maji, hivyo waacheni watape
tape kwanza hadi Oktoba 25, mwaka huu, ndio itakuwa kifo cha UKAWA. Wameingiza
vijana msituni, wanashambulia wafuasi wetu kwenye mikutano, wanaomba kura
kanisani yote hayo hawaoni.”
“Tunafahamu hali yao ni mbaya sana…wamegawanyika
vipande na hawana umoja tena, hivyo wanatafuta sababu za kuonewa
huruma…wakumbusheni kuwa kwa Dk. Magufuli ni kazi tu,” alisema Shaka.
Lowassa,
Sumaye ni
pwagu
na pwaguzi
Katika hatua nyingine Shaka alisema usanii unaofanywa
na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kumnadi mgombea urais wa CHADEMA,
Edward Lowassa, ni sawa na vichekesho vya pwagu na pwaguzi.
Lowassa, ambaye alijiuzulu kwa kashfa ya kampuni ya
kufua umeme ya Richmond, amekuwa akinadiwa na Sumaye anayetajwa kuwa mbadala
kutokana na afya ya mgombea huyo kugubikwa na utata.
Alisema viongozi hao walipewa nafasi za juu ndani ya
Chama na serikali, lakini walishindwa kuonyesha ufanisi na badala yake wengine
wakaondoka kwa aibu.
Alisema wanachokifanya kwa sasa ni kuwalaghai Watanzania
ili wapate nafasi ya kurudi madarakani, jambo ambalo ni ndoto kwao kutokana na
mbinu hizo kubainika.
Alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni
za mgombea ubunge Jimbo la Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia uliofanyika Kijiji cha Mango
Pacha Nne mkoani hapa.
Alisema kinachoonekana kwa sasa kwenye jukwaa la
siasa la CHADEMA ni kituko na kwamba, kamwe hawana ubavu wala dhamira ya kuleta
mabadiliko kama wanavyojinadi.
“Sumaye anapomfanyia kampeni Lowassa awe rais ni sawa
na pwagu kumfanyia kampeni pwaguzi…hawajui wafanyalo kabisa na pia hawafahamu
kuwa hawaheshimiki tena mbele ya Watanzania wanaojitambua.”
“Walipewa nafasi za juu wakashindwa kufanya kazi kwa
ufanisi na sasa wamegeukia upekepeke…wakataeni hawa ni wasanii,” alisema Shaka.
Alisema Sumaye akiwa Waziri Mkuu alisababisha halmashauri
nyingi nchini kupata hati chafu kwa mujibu wa ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG) hivyo hana jipya na la kujivunia mbele ya
Watanzania.
Shaka aliwaomba wananchi wa Mtwara Vijijini kumchagua
Hawa kwa kura nyingi ili aendelee kuwatumikia na kamwe wasikubali ghiliba za
upinzani.
Alisema Hawa ni mwadilifu na ameonyesha uwezo mkubwa
katika kusimamia kazi za serikali na ameongoza TAMISEMI kwa mafanikio makubwa
huku akizuia vitendo vya wizi, ufujaji wa fedha za miradi kwenye halmashauri.
“Huyu ni mwanamke wa shoka, hodari na makini, msikubali
kupoteza hazina hii inayotegemewa na taifa…mpigieni kura kwa sababu ni mwadilifu
na makini,” alisisitiza Shaka.
No comments:
Post a Comment