Saturday, 19 September 2015

CCM NA KIMBUNGA CHA USHINDI, KILA KONA NI MAGUFULI MAGUFULI MAGUFULI!


Macho na masikio ya watanzania yameelekezwa kwa John Pombe Magufuli mwanasiasa anayepewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha mbio za urais. Kiongozi huyo anayeegemea zaidi utendaji kuliko siasa ni mtu wa kujishusha na asiyependa kujishughulisha na mambo makuu.
Anachozingatia katika maisha yake ni moyo wa utumishi. Mwanasiasa huyo aliyewahi kufanya kazi kwenye kiwanda cha Nyanza Cooperative Union kama mkemia, amejizolea heshima na umaarufu kwa sababu ya kuchapakazi na kutetea haki za wengine. Ni mtu anayechukizwa na rushwa, dhuluma, unyonyaji, ubaguzi au upendeleo wa aina yoyote.
Magufuli ni mfuatiliaji wa mambo na msimamizi mzuri wa sheria na taratibu zote za kiutendaji. Mwanasiasa huyo aliyejaliwa kipaji cha kuzungumza kwa ufasaha karibu kabila zote za nchi hii ni mtu asiyenunulika. Msimamo wake usioyumba hasa katika utekelezaji wa maazimio ya serikali umempa mashabiki na wafuasi wengi. Magufuli si mtu mwenye maamuzi magumu kama baadhi ya wanasiasa wasio makini walivyo, badala yake ni mtu makini na mwenye maamuzi sahihi yenye kuwanufaisha watanzania wote.
Magufuli amegeuka lulu na mshumaa wenye mwanga mkubwa kwa watanzania. Wachambuzi wa mambo na wanazuoni wanamuona kama kiongozi pekee anayebeba matumaini na hatima ya taifa letu. Kiongozi huyo anayeongozwa na moyo wa upendo na unyenyekevu amekuwa akiwasihi watanzania kutanguliza utaifa kwanza.
Kadhalika amekuwa akisisitiza kwamba maendeleo ya nchi hii ni lazima yawanufaishe watanzania wote bila kujali tofauti zao za kisiasa. Kwa kutumia Ilani ya Uchaguzi kama mwongozo mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Magufuli anaamini katika Tanzania mpya yenye neema na mabadiliko yaliyo bora na si bora mabadiliko. Katika mikutano yake ya kampeni inayofurika umati mkubwa wa watu amendelea kusimamia azma yake ya kupunguza kodi ya vifaa vya ujenzi ili kuwawezesha watanzania wote kujenga nyumba bora zenye gharama nafuu.
Kadhalika mkombozi huyo mpya wa Tanzania ameweka bayana nia yake ya kuimarisha sekta ya miundombinu na huduma za kiuchumi kama vile Utawala wa Ardhi, Mipango Miji, Ujenzi wa Nyumba na Majengo ya Serikali na Utayarishaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi. Mambo mengine aliyoahidi kuyashughulikia ni pamoja na Upimaji na Ramani, Uendelezaji wa Mipango miji na vijiji pamoja na eneo nyeti la Usafirishaji na Uchukuzi.
Magufuli ambaye alifanya vizuri kwenye Wizara ya Ujenzi ameendelea kufafanua kwamba katika kipindi cha mwaka 2015-2020 CCM itaielekeza Serikali kuendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja, vivuko, nyumba na majengo ya serikali kwa lengo la kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na huduma za kijamii.
Zaidi ya hayo ameendelea kueleza kuwa kipaumbele katika ujenzi wa barabara kitazingatia barabara zinazounganisha nchi yetu na nchi jirani, barabara zinazounganisha mikoa na barabara zinazokwenda kwenye maeneo yenye fursa za kiuchumi kama vile Liganga, Mchuchuma na maeneo mengine ya aina hiyo.
Msingi wa kupendwa na kukubalika kwa Magufuli unatokana na uadilifu na juhudi zake za uchapakazi. Kisaikolojia tayari idadi kubwa ya watanzania wanamuona kama rais anayesubiri kuapishwa na ambaye atamudu vema jukumu hilo zito na nyeti la ukuu wa nchi. Watanzania wa leo si mbumbumbu! Wanapaswa kumfahamu kwa undani rais ajaye wa nchi yetu.
Hawataki kubahatisha kwa kuchagua rais kwa ushabiki au mihemko ya kisiasa. Ni jambo lililo dhahiri kwamba Magufuli ni kiongozi mtulivu, asiye na jazba wala papara. Huyu ndiye chaguo la Mungu na chaguo la watanzania kama rais ajaye wa awamu ya tano. Ni mtu wa watu na kipenzi cha watanzania. Falisafa anayotumia ya “HAPA KAZI TU” inasadifu tabia yake ya kuchapa kazi na azma yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya wachapakazi. Magufuli anataka kila mtu achape kazi. Hataki ubabaishaji, majungu au uzembe. Kwa lugha nyingine Tanzania ya Magufuli itakuwa yenye mabadiliko bora na kwamba mabadiliko hayo yataletwa na watanzania wenyewe kwa kufanya kazi kwa bidii.
Kimbunga cha ushindi wa CCM kinazidi kuvuma huku kikimpeperusha kwa kasi Magufuli kuelekea Ikulu. Dalili zote zinaonyesha kwamba Magufuli atashinda urais tena kwa kishindo. Ama kweli mungu huwafedhehesha wenye kiburi na kumpa amtakaye. Nyota ya Magufuli inang’ara na itazidi kung’ara na wanaojaribu kuizima watazimika wenyewe.
Chama Cha Mapinduzi kinazidi kuimarika na wanaojaribu kukibomoa watabomoka wenyewe. Kwa sasa jina la Magufuli limeingia kwenye rekodi ya siasa za Tanzania. Jina lake limegeuka wimbo midomoni mwa watanzania. Sura yake imegeuka nembo ya haki na alama ya uchapakazi. Lafudhi yake ya kisukuma imezidisha upendo, utani na mshikamano baina ya wasukuma na makabila mengine huku usemi wa “mzigo mzito mpe msukuma” ukizidi kutawala.
 Mikutano ya Kampeni za Magufuli imetawaliwa na sera, hoja, utani, furaha na vichekesho vya hapa na pale huku wasanii mahiri wakiongozwa na TOT, Diamond, Shilole, Ally Kiba, Matonya, Bushoke, Lina, Wema Sepetu, The Original Comedy, Chege, Temba, Kitale na wengineo wakinogesha zaidi mikutano hiyo hasa kwenye miji mikubwa.
Ni ajabu na kweli kila mtanzania anataka kumshika mkono Magufuli ukiachilia kuiona sura yake. Ni jambo la kutia faraja kuona kwamba watanzania wanaunganishwa na Magufuli kupitia mikutano yake ya kampeni. Katika mikutano hiyo wananchi wanapata fursa ya kusikiliza sera za CCM, wanapata fursa ya kufahamiana, wanapata fursa ya kupata elimu na kujifunza mambo mengi. Jambo kubwa zaidi ni kwamba wananchi wakiwemo vijana wanapata pia fursa ya kupata burudani na ujumbe kwa njia ya nyimbo unaotolewa na wasanii.
Huyu ndiye John Joseph Pombe Magufuli “mzee wa Tingatinga” ambaye wakati mwingine amekuwa akiwavunja mbavu wananchi kwa kuwaomba wakumbuke jina la Pombe wakati wa kumpigia kura kwa vile pombe ni kinywaji kinachopendwa na wengi.
Mwanasiasa huyo mwenye vichekesho na utani mwingi hana masihara hata kidogo unapofika wakati wa kazi. Ni mtu asiyezoeleka wala kutabirika. Maadui zake wakubwa ni wavivu, wazembe, wala rushwa, mafisadi na wote wanaokwamisha juhudi za kuliletea maendeleo taifa letu. Kinyume chake marafiki zake wakubwa ni wachapakazi, wazalendo na wote wanaoitakia mema nchi yetu.
Tabia na hulka yake hiyo ya uzalendo kwa nchi imempandisha chati na huenda baada ya kuwa rais wa nchi yetu ataingia kwenye orodha ya viongozi bora na maarufu kabisa duniani. Kimsimamo namfananisha Magufuli na rais wa China Xi Jinping. Magufuli na Ping ni wachapakazi wa kweli wanaokubalika na mataifa yao. Sina shaka baada ya Magufuli kushinda urais, uhusiano baina ya Tanzania na China utazidi kuimarika. Magufuli anastahili kuwa rais wa Tanzania, shime tumpe kura zetu!
Amos Siyantemi
0655689461
0754689461
0689433733

No comments:

Post a Comment