Na Doto Magori
AKIZUNGUMZA Jumanne kwenye hafla ya
taasisi ya Twaweza, kutangaza matokeo ya utafiti wake kuhusu hali ya kisiasa
nchini juzi, jijini Dar es Salaam, mwanaharakati Maria Sarungi katika tathmini
yake, alisema jina la mgombea wa CCM wa urais, Dk John Magufuli, linafahamika
sana kutokana na kujitangaza zaidi.
Alisema misuli ya kifedha iliyonayo CCM
ndiyo inafanya kuweza kujitangaza zaidi kupitia mabango na vyombo mbalimbali
vya habari, kwa maana ya magazeti, redio na televisheni.
“Ukienda sehemu mbalimbali nchini na
hasa vijijini, hukosi kukuta mabango ya Magufuli na hivyo ukimhoji mtu nani
unadhani anafaa kuwa Rais na hata kama hujamtajia majina, atamtaja
Magufuli…lakini hata hivyo matokeo haya si utabiri wa matokeo ya uchaguzi,”
alisema Maria.
Kauli yake ilitokana na ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, kwamba katika swali la unadhani nani anafaa
kuwa Rais, hakukuwa na jina lililotajwa, ila kura zilikwenda kwa Magufuli na
Edward Lowassa, anayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ni kweli kuwa CCM ina misuli kuliko
Ukawa, licha ya umoja huo kushirikisha vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi,
CUF na NLD, huku vitatu vya mwanzo vikipata ruzuku ya serikali kutokana na kuwa
na wabunge.
CCM ina miradi mingi ambayo ni vyanzo
vyake vya fedha, ingawa hilo halikatazi vyama vingine kuwa na miradi kama hiyo,
pamoja na ndani ya vyama vya siasa kuwapo viashiria vya ulaji, huku tukisikia
malalamiko kuwa baadhi ya viongozi wanapokea fedha za ruzuku na misaada mingine
kutoka nje na kuishia mifukoni wao.
Bila shaka Ukawa baada ya kubaini kuwa
hali yake ya kifedha ni hoi na kwamba huenda ikasuasua katika kukamilisha
kampeni kabla ya upigaji kura Oktoba 25, mwaka huu, ikaamua kuitisha harambee
iliyofanyika Dar es Salaam, ambapo taarifa zilisema ilihudhuriwa na watu 800.
Harambee hiyo ilikusanya jumla ya Sh
milioni 97, kwa mchanganuo kuwa Sh milioni 67, zikiwa ni ahadi ndani ya ukumbi,
Sh milioni 20, zikichangwa kwa njia ya simu na Sh milioni 10, zikikusanywa papo
hapo ukumbini chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Ukawa na Chadema, Freeman
Mbowe.
Mbowe akiongoza harambee hiyo,
aliwajulisha washiriki kuwa tangu waanze kampeni, Ukawa wamekuwa wakisaidiwa na
Watanzania mbalimbali wenye nafasi zao (kiuchumi), baadhi wakijitolea magari
kwa ajili ya usafiri wa kampeni.
Alichoshangaza ni kutangaza kuwa kuna
wafanyabiashara watano wenye uwezo mkubwa ambao hawakutaka watajwe majina,
ambao wamekubali kuisaidia Ukawa kwenye kampeni zake kwa siku zilizosalia,
lakini akasema hawakutaka kutajwa majina yao, kwa sababu eti wanaogopa
kufuatiliwa.
“Wakati tunaendelea na uchangiaji hapa,
nimepokea simu kutoka kwa rafiki zangu watano wenye uwezo mkubwa kiuchumi.
Wameahidi kuchangia harambee, lakini wanaogopa kujulikana kwa kuhofia mkono wa
Serikali,” alisema Mbowe.
Akaendelea huku akisikitika:
“Inasikitisha Mtanzania mwenye uhuru ndani ya Taifa lake anahofia kuchangia
safari ya mabadiliko kwa sababu ya kuogopa serikali, wakati serikali iliyopo
imejaa mafisadi wakubwa.”
Kama alichokisema Mbowe si danganya
toto, basi kuna tatizo miongoni mwa wafanyabiashara wanaoogopa kuichangia Ukawa,
lakini pia na viongozi wetu, kwa sababu inawezekana kuogopa kumchangia jambazi
au muuaji akafanye uhalifu kuliko kuchangia watu wema. Je, Ukawa ni miongoni
mwa majambazi hao?
Hii ina maana kuwa wafanyabiashara hao
wakichangia Ukawa, itasababisha matatizo katika nchi, hiyo bila shaka ndiyo
imani waliyonayo nao wakajulikana kuwa wamechangia, la sivyo kwa nini
wanajificha kwa madai kuwa Serikali itawabana? Inashangaza na kuacha maswali ya
Ukawa inashirikiana na wafanyabiashara gani?
Umoja ambao unajumuisha mawaziri wakuu
wawili wa zamani ndio sasa unashirikiana na wafanyabiashara watano wanaoogopa
kujulikana kuwa wametoa mchango kusaidia umoja wa vyama vya siasa? Ni wapi
pameandikwa kuwa wanakatazwa? Kwa nini wanajihisi hivyo na viongozi hao akiwamo
aliyekuwa Mkuu wa Upinzani Bungeni?
Naunga mkono kauli na hoja ya
mwanaharakati wa mtandao wa TGNP, Gemma Akilimali, ambaye alipohojiwa
alishangaa kauli ya Mbowe na kuhoji mbona mfanyabiashara Mustafa Sabodo amekuwa
akiichangia Chadema na kujitangaza bila matatizo na hakupata kufuatwa na
serikali?
“Sabodo ni mfanyabiashara mkubwa tu na
amekuwa akiwachangia Chadema na CCM waziwazi bila kificho na hatujaona lolote
likimtokea. Hivyo hofu zao zinaweza kutujengea maswali katika uwazi wa shughuli
zao,” alitanabaisha Akilimali.
Ni dhahiri kuwa kujificha katika
harambee inamaanisha fedha walizonazo wafanyabiashara hao ni haramu na
wanaogopa kuulizwa walizipata vipi na wapi na pengine hata kodi wamekuwa
hawalipi. Je, ndio wale waliokuwa wakimchangia Lowassa na kupeleka makanisani
akitaja kuwa ni “za marafiki zangu”?
Kuna watu wenye uwezo wao huenda katika
nyumba za ibada na kutoa sadaka za mamilioni ya fedha, lakini hatujasikia hata
siku moja Serikali ikiwafuata na kuwahoji sababu za kufanya hivyo, iweje leo
wafanyabiashara hao wakubaliane kwa pamoja kwamba watachangia, lakini
hawatataka kutangazwa.
Hapa kuna fumbo tata, pengine hawapo na
kama wapo ni wezi au fedha hizo zinatoka kwingine hata nje ya nchi, lakini
wanasingiziwa wafanyabiashara hewa ili kuzihalalisha. Ni vizuri pia hata kiasi
cha fedha kingetajwa kwa sababu ni ahadi tayari kuliko kuficha, kwani wana
Ukawa huenda wasijue ziliingia lini na kutumikaje.
Angalau hilo ni tatizo sugu lililoko
ndani ya Chadema. Waliokikimbia chama hicho wanajua na waliomo wanajua, lakini
wanachelea kulisema, kwa sababu wanajua pia nini kiliwakuta waliolijua
wakalisema hadharani.
No comments:
Post a Comment