NA WAANDISHI WETU
MAKAMU Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, John Malecela, amesema makada wachache wachafu
waliokuwa wakikitia doa Chama na kujali maslahi yao binafsi, wameondoka.
Amesema hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa CCM sasa kitabaki
na wanachama makini, waaminifu na wenye sifa, baada ya makapi kukimbilia
upinzani kuendeleza wimbi la kusaka maslahi binafsi na kukata kiu ya uroho wa
madaraka.
Aidha, amesema mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli,
ndiye chaguo sahihi la Watanzania kwa sasa kwani, ni mchapakazi na atayeleta
mabadiliko ya kweli na ambayo Watanzania wanayahitaji na si porojo za wapinzani.
Amesema ana imani kubwa Dk. Magufuli atapata ushindi wa
kishindo dhidi ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward
Lowassa, anayegombea kupitia CHADEMA.
Mzee Malecela, ambaye kwa muda mrefu alikuwa kimya,
aliyasema hayo jana nyumbani kwake Dar es Salaam, alipozungumza na UHURU katika
mahojiano maalumu.
Alisema huu ni wakati muhimu kwa Watanzania na kuwaasa
kuhakikisha wanachagua kiongozi bora na asiye na uchu wa madaraka kwa kuwa kuna
wengine wanalazimisha kuingia Ikulu kwa nguvu wakati hawana uwezo na sifa.
“Kuna viongozi waliopoteza utu wao kwa kuhama CCM na
kuingia kwenye genge ambalo halina sera wala dhamira ya kuwatumikia Watanzania
zaidi ya kuangalia matumbo yao. Hawa ni wa kuogopwa na kukataliwa hadharani
kabisa bila kificho.
“Sina shaka na Dk. Magufuli na Chama kimechagua mtu
ambaye alikuwa akihitajika kwa maendeleo ya Tanzania. Ninamfahamu na
ninamwamini,” alisema.
Alisema Dk. Magufuli ameitumikia serikali kwa miaka 20,
anafahamu matatizo ya Watanzania wanyonge kwani, licha ya kuwa waziri miaka
yote hiyo hakuwa mtu wa kujikweza wala kuishi maisha ya kifahari.
HOFU
YA VURUGU
Hata hivyo, Mzee Malecela alionyesha hofu kuwa genge la
UKAWA huenda likaanzisha vurugu kutokana na dalili za mgombea wao kushindwa
kuonekana mapema.
Amesema Lowassa hana ubavu wa kupambana na Dk. Magufuli
kwa kuwa tayari ana kashfa na haonekani kuwa imara kiafya, tofauti na mwenzake
ambaye anakubalika kila kona.
Pia, amesema njia nyingine ambayo huenda ikatumiwa na UKAWA
ni kupanga mikakati ya kuahirishwa kwa uchaguzi.
“Hawa tayari wameshikwa pabaya…mgombea wao hana sifa za
kumshinda Dk. Magufuli na wenyewe kwa wenyewe ni vurugu humo ndani wakigombea
madaraka.
“Wameshindwa kufikia malengo waliyojiwekea katika hatua
za mwanzo tu, sasa ikitokea wakapewa nchi si watapigana wakitaka kugawana
vyumba vya kulala Ikulu,” alisema.
No comments:
Post a Comment