Sunday, 4 October 2015

DK SHEIN AIBOMOA NGOME YA CUF PEMBA

Mgombea Urais wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, akibadilisha mawazo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Ndg. Hamad Mberwa Hamad. Dk Shein akiwa katika ziara yake ya mikutano ya kampeni ya kuomba ridhaa za Wananchi kumchagua kwa mara ya pili kuiongoza Zanzibar.

MGOMBEA nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ameibomoa ngome ya CUF huko Kiungoni Pemba na kuvuna wanachama zaidi ya 40 huku akiwaleleza wananchi kuwa siasa za chuki, fujo na hasama zimeshapitwa na wakati hapa nchini na yeyote atakaezirejesha sheria itachukua mkondo wake.

Hayo aliyasema leo katika Mkutano wa  Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika kiungoni katika Jimbo la  Mgogoni, Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao umehudhuriwa na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Dk. Shein alisema kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar kuna amani na utulivu mkubwa na kuwathibitishia wananchi kuwa amani hiyo imesimamiwa na kuandaliwa na Mwenyewezi Mungu pamoja na vyombo vya dola na Serikali iliopo hivyo si rahisi kuazisha vurugu na fujo.

Alisema kuwa siasa za vyama vingi isiwatenganishe Wazanzibari kwani kila mtu ana chama chake na kuwataka wananchi wasihujumiane wala kufanyiana fujo kwa sababu za itikadi za kisiasa kwani sheria inasema kila mwananchi ana fursa ya kupenda chama anachokitaka.

Dk. Shein alisema hayo baada ya gari ya wafusi wa CCM kupigwa mawe wakati wakirudi mkutanoni Gando na kusisitiza kuwa siasa ya vyama vingi sio fujo ambapo aliwaeleza vijana wanaotaka kuvunja amani ya Zanzibar na kuleta vurugu wakati wa uchaguzi wajue hilo haliwezekani na mwenye nia ya kutafanya ajue kuwa vyombo vya dola na dola viko macho.

Alisema kuwa uchaguzi wa amani ndio unaotakiwa "tunataka Zanzibar iwe na utulivu wakati wote na kusihini watu wote waishi kwa amani na utulivu, Zanzibar na watu wake hawataki fujo",alisema Dk. Shein.


Aidha, Dk. Shein alisema kuwa panapozuka zahama hata ibada hazifanyiki wala jambo lolote la maendeleo na kueleza kuwa mtu yeyote atakaejaribu kufanya fujo hapa Zanzibar atashughulikiwa na kuwataka wananchi kuishi vizuri na kufanya siasa bila ya kugombana pamoja na kufanya kampeni za kistaarabu.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza vijana waliojiunga na CCM na kusema kuwa anaamini kuwa wataungana na vijana wenzano wa CCM kwa lengo la kuiletea maendeleo nchi yao.

Alisema kuwa elimu imeimarika sana, ujenzi wa majengo mapya ya msingi na Sekondari kama Kiuyu Minugwini, kuanzishwa kwa Tawi la Chuo Kikuu Pemba katika chuo cha Penjamin Wilium Mkapa na kusema kuwa huduma za chuo hicho katika miaka mitano ijayo zitaimarishwa.

Kwa upande wa sekta ya afya alisema kuwa Kojani, huduma za meno zitapelekwa kwani  huduma za afya katika Jimbo la Kojani zimeimarika ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za daktari na kuendelea kuahidi kuwa katika miaka miwili ya uongozi wake huduma za fya zitakuwa bure.

Aidha, alisema kuwa katika mwaka wake wa kwanza elimu ya Sekondari nayo itakuwa bure na kueleza kuwa huduma za maji zimeimarika Kangagani na Kiuyu na Shehia zote za Kojani zitapata maji safi na salama katika miaka mitano ya uongozi wake.

Alisema kuwa mji wa Chake, Mkoani na Wete huduma za maji zimeimarika na kiwango cha maji Mkoa wa kaskazini Pemba zimeimarika zaidi hivi sasa na lengo ni ifikapo mwaka 2018 huduma hiyo zitafikiwa asilimia 100.

Alieleza kuwa sekta ya miundombinu ya barabara katika Mkoa huo wa Kaskazini imeimarika kwa kiasi kikubwa na kila pahala katika barabara kuu zimetiwa lani na ni barabara za kisasa na hivi karibuni barabara kutoka Wete hadi Chake itajengwa upya mapema hapo mwakani.

Akigusia sekta ya umeme alisema kuwa sekta hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa na kuahidi kupelekwa umeme katika maeneo yote yaliobaki ndani ya miaka mitano ijayo.

Dk. Shein alisema kuwa mafanikio yote yaliopatikana tokea Mapinduzi yametokana na ASP na CCM, huku akieleza kuwa serikali imekuwa ikiwatekelezea wananchi maendeleo na kuwatumikia bila ya ubaguzi.

Aliwataka wananchi kumchagua kwani ataendelea kuwapelekea maendeleo zaidi.

Pamoja na hayo Dk. Shein alisema kuwa wakati akiomba ridhaa katika uchaguzi uliopita alisema kuwa pindipo wananchi wakimchagua Serikali ya Umoja wa Kitaifa ataiendesha vizuri kwa kufuata taratibu zote ikiwa ni pamoja na sheria na Katiba ya Zanzibar.

Alisema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ameiendesha kwa bidii kubwa na kushangwazwa na kauli zinazotolewa na viongozi wa CUF kuwa chama hicho hakikutendewa haki wakidai kuwa wanataka na wao wawe na Wakuu wa Mikoa na Masheha wakati Katiba haielekezi hivyo.

Katika kuiongoza Serikali hiyo alisema kuwa kila kitu kimefanywa pamoja, na hakuna jambo la kiserikali aliloamua peke yake kwani katika maamuzi huwashirikisha viongozi wote wa ngazi za juu akiwemo  Makamu wa Kwanza wa Rais, Makamu wa Pili pamoja na Wajumbe wote wa Baraza la Mapinduzi.

Dk. Shein alieleza kuwa hata suala la kutafuta ufumbuzi wa Uwamsho baada ya kufanya vurugu walikubaliana na kushaurinana na viongozi wote wa Serikali wakiwemo viongozi wa CUF lakini anashangaa kuwa hilo hawalisemi.

"sina ninaemchukia wala kumuonea kwani hata mimi mwenyewe nafuata sheria... wanajua watashindwa na wanatafuta sababu lakini nawaambia kuwa uchaguzi utafanyika na CCM intashinda.. na mimi nikiwa Rais nitawatumikia wote"

Pamoja na hayo aliahidi kuiimarisha sekta ya kilimo na uvuzi na kuwataka wavuvi wakae mkao wa kula kwa kuanza kuvua kisasa.

"Tutagawa vihori, boti za kisasa, kiwanda kikubwa cha kuvua samaki Unguja kitajengwa na nitamshwawishi muekezaji kuja kujenga kiwanda na Pemba sambamba na kuwapa mitaji wavuvi",alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa Serikali itaagiza matrekta mia moja na tayari mchagkato wa kuja kushughulikia sekta ya uvuvi na washirika wengi wa maendeleo wameahidi kuja kuekeza Zanzibar.

Alieleza kua tokea mwaka 2001 hadi 2010 ameanza kulishughulikia suala la mafuta tokea akiwa Makamu wa Rais hadi hii leo na hakuna hata mmoja atakae sema kafanya yeye.

Alisema kuwa tayari ameshakwenda nchi mbali mbali kwa lengo la kulifanyia kazi suala hilo 2012 mwezi wa Agosti Ras- El Haiman, Uholanzi Kampuni ya Shell na kuja zaidi ya nchi nane nazo zimekuja kuomba mashirikiano hayo.

"Tutayachimba wenyewe kwa sheria zetu... si vizuri kujitokeza mtu mmoja kwa lengo la kutaka asifiwe kwani iliofanya ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar",alisema Dk. Shein.

No comments:

Post a Comment