Wednesday, 7 October 2015

DK. SHEIN KUFUMUA MASHIRIKA YA UMMA, WATENDAJI WAZEMBE KUONDOLEWA





Na Hamis Shimye, Pemba

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), visiwani Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema ataleta mabadiliko makubwa kwenye mashirika mbalimbali visiwani humo ikiwemo kuwaondoa watendaji wazembe kazini.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha mashirika yanajiendesha kwa faida tofauti na sasa, ambapo yamekuwa yakileta hasara.

Akizungumza katika mikutano yake ya kampeni Kusini Pemba, juzi,  Dk. Shein alisema mashirika hayo, likiwemo shirika la meli yamekuwa yakijiendesha kwa hasara jambo linalompa wakati mgumu.

“Hatutaki watu wengi wasiofanya kazi, tunataka tujiendeshe kwa faida, mashirika haya yamekuwa kama watoto tuwalee tu bila mafanikio, hilo haliwezekani," alisema.

Alisema lazima wachukue hatua katika hilo na ndio maana katika miaka yake mitano ijayo, atahakikisha mashirika mengi yanakuwa na faida kubwa.

"Hivi sasa Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC), linafanya vizuri na yule mama anastahili pongezi kwani hivi sasa wao ndio wanaleta fedha serikalini na hawapokei ruzuku serikalini tena,"alisema.

Dk. Shein alisema lazima Zanzibar iwe na watendaji bora na wenye ari, hivyo ndani ya miaka mitano ijayo sio muda wa kuwa tena na watendaji wabovu.


Serikali kuanzisha mahakama ya ardhi

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema ataanzisha mahakama maalumu ya ardhi itakayoshughulikia migogoro ya ardhi.

Amesema miongoni mwa maandalizi ya uanzishwaji wa mahakama hiyo ni pamoja na kuifanyia marekebisho   sheria ya ardhi ili iendane na mazingira ya sasa.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni juzi, Dk. Shein alisema pindi itakapoanzishwa mahakama hiyo, itakuwa na jaji maalumu ambaye atakuwa na kazi ya kusikiliza kesi za ardhi pekee.

Pia, alisema licha ya kuboresha suala hilo, matatizo yaliyoko katika sekta ya elimu visiwani Pemba yataendelea kutatuliwa na kubakia historia.

Dk. Shein alisema serikali yake ijayo itafufua elimu ya watu wazima ambayo imesahaulika kwa muda mrefu.

Hivyo, alisema ataongeza vituo vya mafunzo ya ufundi kutoka 22 vilivyopo hadi 34, lakini pia ili kuongeza ubora wa elimu.


Atakayenunua meli, lazima iwe mpya

SERIKALI ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), imesema kuanzia mwaka ujao, mfanyabiashara yeyote atakayetaka kununua meli lazima iwe mpya.

Pia, imesema itawahamasisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha wanawekeza katika usafiri wa majini.

Hayo yalisemwa juzi na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye pia ni mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, alipokuwa akihutubia Kusini Pemba.

Alisema amejipanga kwa kiasi kikubwa kuboresha usafiri wa majini, ikiwemo kuwavutia wawekezaji na kuwataka wafanyabiashara wanunue meli mpya.

"Kuanzia mwakani hatutaruhusu tena kuingizwa kwa meli zilizochakaa au za siku nyingi  sana. Lazima kila mfanyabiashara anayetaka kuleta meli basi iwe mpya," alisema.

Mbali na hilo, Dk. Shein alisema serikali yake ina mpango wa kuboresha usafiri wa majini kutoka Unguja hadi Pemba.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Omary Yusuph Mzee amesema ana hakika na ushindi wa Dk. Shein.

"Nina uhakika na ushindi wa Dk. Shein na ninawaahidi siku ya kuapishwa kwake nyote mtasafiri bure kuja Unguja na meli mpya,"alisema.

Waziri huyo, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, alisema tayari taratibu za ununuzi wa meli hiyo zimeshakamilika na muda wowote kuanzia sasa itawasili Zanzibar.

Hatutarejesha usultani Z’bar- Dk. Shein

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema wale wenye mawazo kuwa utawala wa kisultan utarudi tena visiwani humo, wanajidanganya.

Pia, amesema Zanzibar tayari inayo mamlaka kamili na ndio maana wana katiba yao pamoja na kujiamulia mambo mengi ya kuleta maendeleo.

Dk. Shein alisema anashangazwa na wanaofanya siasa za kutisha watu na kusisitiza kuwa hatishwi, anachofuata ni sheria.

"Wananchi msiogope na yeyote asikutisheni, chagueni kiongozi mnayemtaka kwani uchaguzi ni sehemu ya demokrasia,"alisema.

Alisema anashangazwa na watu wanaodai mamlaka kamili huku wakijua fika kuwa Zanzibar ni nchi na yenye utaratibu wake.

Dk. Shein alisema mapinduzi ya mwaka 1965 yaliyomtoa sultan yatadumishwa na anayedhani kuwa utawala wa kisultan utarudi tena anajidanganya.

Alisema Hayati Abeid Amaan Karume alifanya mambo mengi hadi kupatikana kwa Mapinduzi, hivyo wao hawawezi kufanya kinyume na hapo au kuvunja Muungano.

Kwa upande wake, mke wa Hayati Karume, Mama Fatma Karume alisema Dk. Shein ameifanyia makubwa Zanzibar na anapaswa kupewa kura nyingi.

Aliwaomba vijana wasidanganywe na wanasiasa katika uchaguzi huu, wampe kura nyingi Dk. Shein kwa kuwa ndiye mtu sahihi kwa sasa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment