MGOMBEA Urais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein,
amewataka wananchi kuendelea kuichagua CCM, kwani ndio inayothamini na
kutekeleza malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Akihutubia mkutano mkubwa wa aina yake wa kampeni
uliofanyika Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja, Dk. Shein, alisema Chama
kitaendelea kuyaenzi Mapinduzi pamoja na Muungano kwa kuweka misingi imara
itakayowanufaisha wananchi wote.
Dk. Shein aliwaambia maelfu ya wananchi waliohudhuria
mkutano huo kuwa wanapaswa kuichagua CCM, kwani ndicho Chama chenye uwezo na
kimeonyesha mfano wa utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi na ahadi za Rais wa
kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume.
“Mapinduzi ndiyo yaliyoweka msingi wa usawa na kuondoa
ubaguzi ambao uliwanyima haki na kuwakandamiza wananchi walio wengi wa
Zanzibar,” Dk. Shein.
Alisema Mapinduzi yalileta usawa na kujenga mazingira ya
kuijenga nchi kwa ushirikiano na kwa umoja na kwa maslahi ya watu wote.
Mgombea huyo alisema Zanzibar ni maarufu ulimwenguni tangu
karne zilizopita, lakini umaarufu huo hautakuwa na manufaa iwapo hawataweza
kulinda na kuienzi amani na utulivu uliopo.
Katika kipindi kijacho, Dk. Shein aliahidi kuimarisha
huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, umeme, maji pamoja na miundombinu ya
barabara ili kukidhi mahitaji makubwa ya huduma hizo kutokana na mji huo kukua.
“Tutaimarisha
huduma za umeme kwa kuweka transfoma kubwa yenye KVA 200, katika mji mpya
ulioko Ras Nungwi, itakayoweza kuhudumia wateja wengi na kwa uhakika
zaidi,”alisema.
Dk.Shein aliwaeleza wananchi hao kuwa biashara ya utalii
ndio inayoipatia Zanzibar fedha nyingi za kigeni, hivyo lengo la serikali
katika miaka mitano ijayo ni kuongeza idadi ya watalii wanoitembelea Zanzibar
na kufika 500,000, ifikapo 2020, kutoka 300,000, hivi sasa.
Alisema Nungwi inaendelea kusonga mbele kwa kujenga
majengo mengi na hoteli nyingi za kitalii.
Dk. Shein alisema akichaguliwa tena, serikali yake
itawajengea uwezo wavuvi nchini kwa kuwapatia boti zenye ukubwa wa kati na
kubwa ili waweze kuvua kwa uhakika na kupata mapato makubwa zaidi.
Kuhusu kilimo cha mwani, Dk. Shein alisema ataiamarisha
soko la mwani kwa kutafuta masoko mapya ya zao hilo ili wakulima waweze kupata
bei nzuri na kufaidi jasho lao.
No comments:
Post a Comment