NA MWANDISHI WETU
MAMBO mazito yameendelea
kuibuka kufuatia kifo cha mwanasiasa mahiri nchini, Mchungaji Christopher
Mtikila, ambapo hivi sasa inadaiwa kifo chake kilipangwa.
Mchungaji Mtikila alifariki
dunia juzi, kwa ajali ya gari, iliyotokea katika kijiji cha Msolwa, Chalinze,
mkoani Pwani.
Wakati utata ukiendelea
kutawala kifo cha Mtikila, Mchungaji Patrick Mgaya, ambaye alikuwa miongoni mwa
watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo, ameibuka na kusema Mungu atalipa damu hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama
cha DP (Tanganyika), Abdul Mluya, alisema chama hicho kimesikitishwa na kifo
cha Mtikila na kwamba, kinaamini kuwa kifo chake kilipangwa.
Alisema chama kimepata
mashaka makubwa na mazingira ya kifo cha mchungaji huyo wa Kanisa la Full
Salvation.
Mluya alisema hayo jana
nyumbani kwa Mtikila, Mikocheni B, Dar es Salaam na kuongeza kuwa wanalitaka
Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kufanya uchunguzi wa kina wa kifo
hicho.
“Ajali ya Mtikila, chama
chetu kinamashaka nayo, hivyo tunavitaka vyombo vya dola, likiwemo jeshi la
polisi kufanya uchunguzi wa kifo hicho,” alisema.
Alisema Oktoba 2, mwaka
huu, Mtikila aliondoka Dar es Salaam kwenda Njombe kwa ajili ya kufanya
mikutano ya kampeni, lakini walipofika njiani gari lao liligonga gari lingine
kwa nyuma.
Mluya alisema mazingira ya
ajali hiyo ilikuwa ya kutatanisha, kwani gari hilo lilionekana kulitegeshea
gari alilopanda Mtikila.
Alisema Septemba 25-26,
mwaka huu, Mtikila alifanya mkutano Bunda Mjini, ambapo alikuwa anafuatiliwa.
Mluya alisema kutokana na
hali hiyo, walimuamisha Mtikila hoteli aliyofikia na kumpeleka kwingine, lakini
kutokana na mazingira yaliyokuwepo, waliamua kumpeleka Mwanza.
Alisema wakati wanaenda
Mwanza, walipofika Serengeti, kulikuwa na gari linawafuatilia, lakini walifika
Mwanza salama.
Mluya alisema siku hiyo Mtikila
alilala Mwanza na asubuhi alikuwa na
mahojiano katika kituo kimoja cha televisheni kilichoko Mwanza.
Alisema kutokana na mambo
mbalimbali aliyokuwa anayaibua Mtikila hivi karibuni, alikuwa anafuatiliwa,
hivyo hata kifo chake hawana imani nacho na kwamba kinaweza kuwa cha kupangwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo
alisema muda mfupi baada ya ajali ya Mtikila, kulikuwa na picha kwenye mitandao
ya kijamii na mpaka sasa aliyezipiga hafahamiki.
Alisema picha hizo
zimeongeza hofu, kwani ziliwekwa kwenye mtandao muda mfupi baada ya ajali na
kwamba huyo aliyeziweka alikuwa sehemu gani wakati ajali inatokea.
Mluya alisema DP,
wataendelea kuenzi matendo yake na mapambano aliyokuwa akifanya Mchungaji Mtikila.
MCHUNGAJI MGAYA
AIBUKA
Mmoja ya watu waliopata
ajali na Mtikila, Mchungaji Mgaya, alisema walikuwa kwenye mkutano wa kampeni
Njombe, lakini wakati mkutano ukiendelea, zilikuja pikipiki mbili zikiwa na
bendera za vyama viwili tofauti.
“Hizi pikipiki zilipita wakati
mkutano ukiendelea zikiwa na bendera za vyama viwili tofauti ambavyo
hakuzitaja.
“Bendera hizo nitazitaja
siku nikiitwa na Mkurugenzi wa Upelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani,” alisema Mgaya.
Alisema wakati wanatoka
kwenye mkutano Njombe, walipofika Mafinga walikutana na gari aina ya Toyota
Land Cruiser, lililokuwa na rangi ya kijivu na muda wote lilikuwa likiwafuatilia.
Mgaya alisema wakati
wanaendelea na safari, wakiwa Mikumi, Mchungaji Mtikila alitaka kujisaidia, hivyo
wasisima.
Alisema wakiwa katika eneo
la Mikumi, mara gari hilo likapita kwa spidi kubwa na muda huo gari lao
likaondoka eneo hilo.
Mgaya alisema walianza
safari, lakini dereva wao alikuwa anakimbiza gari kwa kasi licha ya kuonywa
mara kadhaa na Mtikila kuwa asikimbize, lakini aligoma kupunguza mwendo.
“Yule dereva alidai anataka
awahi kufika Chalinze, ili amkabidhi gari dereva mwingine atulete Dar es
Salaam,” alisema.
Alisema walipofika eneo la
Mdaula waliioona tena ile Cruiser ikiwa mbele kwa umbali wa mita 20, ambapo
dereva wao alikuwa akilikimbiza.
“Tulipofika eneo la ajali,
ile gari ilikuwa mbele yetu pembeni kulikuwa na lori, lakini wakati hiyo cruiser,
ikijaribu kulipita lori, mbele kukatokea lori lingine.
“Nilidhani lori na cruiser litagongana
uso kwa uso, lakini cha kushangaza sikujua ilipitaje na ndipo tukaingia sisi,
tukajikuta gari letu lipo kwenye msingi,” alisema.
Hata hivyo, alisema kuwa simu
ya Mtikila haikuonekana pamoja na kuitafuta kwa muda mrefu baada ya ajali.
Mgaya alisema ni lazima
Mwenyezi Mungu atalipa damu ya Mtikila.
Mwili wa Mchungaji Mtikila utaagwa
leo katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na baadaye utasafirishwa kwenda
Ludewa kwa maziko.
000
No comments:
Post a Comment