NA RACHEL KYALA
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema hadi sasa
imetoa elimu ya mpigakura kwa zaidi ya asilimia 90, tofauti na lawama kwamba
haijaifikia jamii ipasavyo.
Aidha NEC, imesema imeshaendesha vipindi vya
televisheni 22, na 24 vya redio
mbalimbali, huku elimu hiyo ikiendelea kutolewa kwenye redio ya mtandao wa tume
kwa saa 24 hadi sasa na kutoa kibali kwa asasi 447 kutoa elimu hiyo kwa jamii
tangu Agosti 19, mwaka huu.
Vile vile imesema imeshatoa taarifa mbalimbali
magazetini, kuchachapisha majarida ya elimu kwa mpigakura, ambapo wiki
iliyopita ilikutana na wawakilishi wa makundi mbalimbali, ikiwemo walemavu,
vijana na wanawake.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Habari na Elimu kwa
Mpigakura, Giveness Aswile, alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam na kuongeza
kuwa NEC inawashangaa wanaoibeza kwamba
haijatoa elimu ya kutosha.
Alizishangaa taasisi kama vile Mtandao wa Asasi za
Kiraia wa Kuangalia Uchaguzi Tanzania (TACCEO).
Mtandao huo katika mkutano wake na waandishi wa
habari jana, uliitupia lawama NEC kuwa
imetoa elimu ya mpigakura kwa asilimia 8.6 tu, jambo ambalo ulidai utawakosesha
watu wengi haki ya kupiga kura.
“Tatizo watu wanachanganya elimu ya uraia na elimu
ya mpigakura na kuipa NEC, majukumu yasiyo yake, NECc imeshafanya sehemu yake
kwa kiasi kikubwa na bado inaendelea, madai hayo hayana tija yoyote,” alisema
Giveness.
Alisema, elimu ya mpigakura inapaswa kuelimisha
namna mpigakura anavyotakiwa kushiriki katika uchaguzi, maeneo ya kupgia kura,
huku elimu ya uraia inaelimisha wajibu, sababu na haki za kupiga kura.
“Elimu ya mpigakura ni kipengele kidogo tu ndani ya
elimu ya uraia, ambapo serikali hadi sasa bado haijaunda chombo maalumu cha
kutoa elimu hiyo, hivyo suala hili ni mtambuka ni wajibu wa wadau wote, ikiwemo
vyama vya siasa,” alisema.
Katika hatua nyingine, alisisitiza kuwa vituo vya
kupigia kura ni vile vile ambavyo vilitumika kuandikisha wapiga kura na kusema watu
wote wanapaswa kurudi nyumbani wanapomaliza kupiga kura.
No comments:
Post a Comment