Monday 19 October 2015

USHINDI WANGU UTAKUWA WA TSUNAMI-DK MAGUFULI


Na Rashid Zahor, Geita

MGOMBEA urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema kutokana na kukubalika kwake katika mikoa yote aliyokwenda kufanya mikutano ya kampeni, ana uhakika wa kupata ushindi wa tsunami katika uchaguzi wa mwaka huu.

Amesema katika mikoa yote aliyokwenda kufanya kampeni, wananchi wamemkubali na kumuhakikishia kumpigia kura nyingi ili aweze kuwa Rais wa awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Ushindi wa mwaka huu ni wa tsunami. Kote nilikokwenda wananchi wanasema ni Magufuli. Wapinzani wataisoma namba. Wao ni wasindikizaji tu," alisema Dk. Magufuli jana, alipohutubia mkutano wa kampeni, uliofanyika kijiji cha Nkome, Jimbo la Geita Vijijini, mkoani Geita.

Aidha, akihutubia mkutano uliofanyika Nyehunge, Jimbo la Buchosa, Wilaya ya  Sengerema mkoani Geita, mgombea huyo aliwataka Watanzania wasikubali kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa kisingizio cha kuuchukia umasikini.

Alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakijinadi kuwa wanauchukia umasikini, lakini ndio walioifilisi nchi na kuifikisha mahali ilipo na kuwafanya wananchi wake wawe masikini.

Amesema wanasiasa wa aina hiyo hawapaswi kupewa uongozi wa nchi kwa sababu hawana uwezo wa kuiletea nchi maendeleo zaidi ya kutaka kujinufaisha wao binafsi.

Akihutubia mkutano huo huku manyunyu ya mvua yakinyesha, Dk. Magufuli alisema wapo wanasiasa wanaodai kuwa serikali haijafanya lolote kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita, wakati baadhi yao walikuwa mawaziri wakuu wa serikali mbili tofauti na pia washauri wakuu wa rais.

"Hawa ndio waliotucheleweshea maendeleo. Wanadai kwamba serikali haijafanya lolote, wakati waliwahi kuwa viongozi wa serikali. Na wanadai kwamba wanauchukia umasikini," alisema mgombea huyo na kuzielezea kauli hizo kuwa ni sawa na kuwauzia wananchi mbuzi kwenye gunia.

Alisema binafsi licha ya kuwa waziri kwa miaka 20, hakuwahi kupokea rushwa ama kutaka kutajirika, japokuwa wizara yake ilikuwa ikihusika kutia saini mikataba yenye fedha nyingi kuliko wizara zingine.

Alisema umasikini wa Watanzania na kiu ya kuwaletea maendeleo ni miongoni mwa mambo yaliyomshawishi na kumfanya ajitose kuwania urais wa Tanzania kwa lengo la kuwaletea maendeleo.

Dk. Magufuli alisema baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani wamekuwa wakijinadi kuwa watatoa kila kitu bure kwa wananchi, lakini hawaelezi watatumia njia zipi kuzifanya huduma hizo ziwe za bure.

Aliwataka wananchi iwapo watapewa pesa na wapinzani siku ya kupiga kura, Jumapili ijayo, wazipokee na kuzila, lakini kura zao wazielekeze kwa wagombea wote wa CCM.

"Msichague watu wasiokuwa na uchungu na wananchi. Mabadiliko ya kweli ni kufanyakazi na kuwasaidia Watanzania walio masikini,"alisema mgombea huyo huku akishangiliwa na wananchi hao, ambao hawakujali manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakiwanyeshea.

Alisema ishara zinazotolewa na wapinzani za kuzungusha mikono hewani kama watu wanaoendesha baiskeli au pikipiki, haziwezi kuwaletea mabadiliko. Alisema shida ya Watanzania sio vyama vya siasa, bali wanataka maendeleo.

Aidha, Dk. Magufuli alisema uamuzi wake wa kufanya kampeni kwa kutumia barabara umelenga kufika katika maeneo mengi nchini na pia kushuhudia kero zinazowakabili wananchi ili aweze kuzitafutia ufumbuzi.

Aliwaahidi wananchi wa Bushosa kuwa atakapoapishwa na kuwa rais wa Tanzania, atatoa kipaumbele kwa ujenzi wa barabara ya Kamanga hadi Sengerema kwa kiwango cha lami.

Hata hivyo, aliwataka wavuvi katika jimbo hilo na mkoa wa Geita, kujiepusha na uvuvi wa kutumia sumu aina ya thiodan kwa vile unasababisha kutoweka kwa samaki kwenye Ziwa Victoria.

Alisema samaki mmoja aina ya sangara anakuwa na mayai zaidi ya milioni moja na nusu, hivyo anapouawa kwa sumu ni sawa na kupoteza idadi hiyo ya samaki.

Aliwataka wavuvi hao kutunza mazalia ya samaki kwa kuwa iwapo wataendelea kuwaua kwa sumu, watakosa kazi ya kufanya siku zijazo na hivyo kudumaza maisha yao.

"Japokuwa nimekuja kuwaomba kura, lakini lazima niwaambie ukweli. Tumepewa ziwa hili na Mungu, lazima tulitumie vizuri," alisema.

Kabla ya kufika Bushosa, msafara wa Dk. Magufuli ulisimamishwa katika vitongoji vinane, kutokana na wananchi kuwa na kiu ya kumuona na kusikiliza sera zake. Vitongoji hivyo ni Kamanga-Kivukoni, ambako msafara wake ulianza saa 3.30 asubuhi.

Msafara wa Dk. Magufuli pia ulisimamishwa katika vitongoji vya Nyamatongo, Katungulu, Kasenyi, Nyamazugo, Ruchili, Bukokwa na Kalebezo.

Akiwa Kalebezo, Dk. Magufuli alisema amefurahi kufika tena katika kitongoji hicho kwa sababu ndiko alikobatizwa katika Kanisa la Kalebezo.

AZURU MAKABURI YA BABU NA BIBI YAKE

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli, jana alitembelea kwenye makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini na kufanya ibada ndogo ya kuwaombea dua.

Dk. Magufuli alifika nyumbani kwa babu yake saa 6.30 mchana na kupokewa na baba yake mdogo, Michael Magufuli, kabla ya kupelekwa kwenye makaburi hayo, ambako aliongoza ibada ndogo ya kuwaombea dua.

Akizungumza kwenye eneo hilo, Michael alisema makaburi hayo ni ya babu na bibi wa mgombea huyo pamoja na ndugu zake wengine, waliofariki dunia miaka mingi iliyopita.

Michael alisema asili ya ukoo wa Dk. Magufuli ni Katoma, ambako ndiko baba yake alikozaliwa kabla ya kuhamishia makazi yake Chato.

"Tumezoea kumuona ndugu yetu kwenye tv na kumsikiliza kwenye redio, leo tumefurahi kumuona yeye mwenyewe,"alisema na kuongeza kuwa wanamuombea dua kwa Mungu ili aweze kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema amefarijika kufika tena katika eneo hilo kwa sababu ndiko alikozaliwa na kukulia na pia ndiko ukoo wake ulikoanzia.

Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwatambulisha ndugu zake kwa wanahabari kabla ya kuingia kwenye nyumba ya familia, iliyoko umbali wa mita 30 kutoka barabara itokayo Kamanga kwenda Sengerema.

Mgombea huyo alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake, aliyemtaja kwa jina la Anastazia, siku alipoivisha pombe yake.

Alisema babu yake, marehemu Michael, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 1.3 baada ya kumuuguza kwa muda mrefu akiwa Dar es Salaam na baadaye kumrejesha Katoma.

"Kwangu siku hii ni ya pekee. Nilipojua kwamba nitasafiri kwa kutumia njia hii, niliona ni lazima nipite hapa kwa sababu ndiko maisha yangu yalikoanzia,"alisema Dk. Magufuli na kusifu maendeleo yaliyopatikana katika kijiji hicho, ikiwemo nishati ya umeme.

Aliwaomba wakazi wa kijiji hicho wamuombee dua kwa Mungu ili aweze kushinda kiti cha urais, katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika nchi nzima Jumapili.

Akihutubia mkutano uliofanyika kijiji cha Nkome, Jimbo la Geita Vijijini mkoani Geita, mgombea huyo alisema mikutano aliyoifanya katika mikoa yote nchini, imemuhakikishia kupata ushindi wa tsunami katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alisema kote alikokwenda, wananchi wamemuhakikishia kumpigia kura kwa wingi kutokana na kuvutiwa na sera zake, hivyo kumuhakikishia ushindi wa kishindo, ambao  ameufananisha na tsumani.

Aidha, mgombea huyo alisema serikali yake itaboresha uvuvi wa samaki katika Ziwa Victoria kwa kuwakopesha wavuvi zana za kuvulia samaki.

Alisema lengo la serikali yake ni kuona wavuvi wanafanya biashara na kutajirika, tofauti na ilivyo sasa.

Aidha, alisiema serikali yake imepania kufufua viwanda vyote vilivyokufa ili kuongeza ajira kwa vijana na pia kuongeza bei ya zao la pamba ili wakulima waweze kunufaika na kilimo cha zao hilo.

Aliyataja malengo mengine ya serikali yake kuwa ni kuongeza thamani ya matunda yanayolimwa hapa nchini kwa kujenga viwanda vya juisi ili kuondokana na ununuzi wa juisi kutoka nje ya nchi.

"Haiwezekani tukaendelea kuagiza juisi kutoka nje. Ninaposema serikali yangu itakuwa ya viwanda, hiyo ndio dhamira yangu,"alisema.


No comments:

Post a Comment