ALIYEKUWA
Spika wa Bunge la Tisa, Samwel Sitta, amesema bunge lijalo, linalotarajiwa
kuanza vikao vyake Novemba 17, mwaka huu, linapaswa kutawaliwa na hoja za
msingi na si wabunge kupiga kelele.
Kutokana
na changamoto zinazotarajiwa kulikabili bunge hilo, Sitta amesema anahitajika
mtu mwenye uzoefu na anayezifahamu vyema kanuni za bunge ili kutenda haki baina
ya Chama tawala na upinzani.
“Wakati
umefika wa bunge lijalo kuwa la kujenga hoja na sio wabunge kupiga
kelele,”amesema.
Sitta,
alisema hayo jana, katika mahojiano maalumu na kipindi cha Hello TZ,
kinachorushwa hewani na kituo cha Radio Uhuru FM cha Dar es Salaam.
Katika
mahojiano hayo, Sitta aliweka wazi nia yake ya kugombea nafasi ya uspika katika
Bunge la 11 na kuongeza kuwa, ameamua kuwania nafasi hiyo baada ya kuona
changamoto zilizopo baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
“Kuna mambo ambayo huwezi kuyafanya ukiwa
pembeni, bali ujuzi wako mahususi unahitajika hata kama unakwenda unaachia pole
pole. Kama suala ni kurithisha uzoefu, litapatikana humo humo,” alisema
Aidha,
alisema umakini unahitajika katika bunge la 11 kutokana na kiporo cha Katiba Inayopendekezwa
na kuongeza kuwa, anafahamu vizuri kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye katiba hiyo.
“Katiba
ya nchi huangusha nchi, ni suala ambalo
lisipowekwa vizuri,
lisipotengenezewa
mazingira mazuri ya kwenda mbele, linaweza kutugawa tukafika mahali ambapo
mambo mengine yasikae vizuri,” alisema.
Alisema
anazielewa hisia za pande zote mbili kuhusu Katiba Inayopendekezwa na kwamba,
anaamini ana uwezo na sifa za kupata nafasi hiyo ya uspika na ataifanya vizuri
atakapopata nafasi ya kuliongoza Bunge la 11.
Alisema
kuna mambo mengi ndani ya Katiba Inayopendekezwa yanayohitaji umakini wa hali
ya juu na kutolea mfano wa suala la mgombea binafsi, linalohitaji kuwekewa
sheria ili kutoa mwongozo katika nafasi hiyo.
“Suala
la mgombea binafsi linahitaji kuwekewa sheria. Kama ni chama mnaambiwa kabisa
mkileta ukabila, udini na ukanda, chama kinafutwa je, kwa mgombea binafsi inakuwaje?”
Alihoji.
Aliongeza
kuwa iwapo atapata nafasi hiyo, atahakikisha anamaliza vizuri jambo hilo ili
kila Mtanzania aridhike na maamuzi yatakayotolewa na bunge.
Sitta
alisema ndani ya miaka mitano, watu wanategemea maendeleo na mabadiliko ya katiba ili nchi iendelee kubaki
na umoja na amani na waridhike kwamba haki itatendeka ndani ya katiba mpya.
Alisema
kinachohitajika katika bunge lijalo ni uvumilivu na kuyakusanya makundi yote yafanye
kazi kwa pamoja na kujenga bunge la kizalendo.
“Tunahitaji
bunge litakalotanguliza maslahi ya nchi kwani uchaguzi umeshamalizika,
tusijenge hisia miongoni mwa majirani zetu katika Afrika kwamba kila tunachokifanya
tunakidharau, tujenge taifa moja la kizalendo,” alisema.
Sitta
alisema anachosubiri ni taratibu za Chama ili aweze kuchukua fomu ya kuomba
kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.
Kwa
upande wake, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye,
alisema mpaka sasa Chama hakijapanga ratiba ya uchukuaji fomu za kuomba
kuteuliwa na chama hicho kwa ajili ya nafasi hiyo ya uspika.
Sitta,
aliongoza bunge la tisa kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia 2005 hadi 2010,
na kupewa jina la ‘Mzee wa Kasi na Viwango.’
No comments:
Post a Comment