Friday, 4 December 2015

PROFESA LIPUMBA AACHIWA HURU


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemwachia huru aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi 30 wa chama hicho, waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko usio halali.

Washitakiwa hao waliachiwa huru jana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi, baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashitaki.

“Kwa mamlaka aliyonayo Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya washitakiwa, hivyo tunaiomba mahakama iondoe kesi,” aliomba Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi.

Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo, Hakimu alisema kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka hana nia ya kuendeleza mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili washitakiwa, hivyo anawaachia huru na kuwatakia maisha mema.

Mbali na Lipumba, washitakiwa wengine walioachiwa huru ni Shabani Ngurangwa, Shabani Tano au Kasakwa, Shabani Polomo, Juma Mattar, Mohammed Kirungi, Athumani Ngumwai, Shaweji Mohamed na Abdul Juma.

Wengine ni Hassan Saidi, Hemed Joho, Mohamed Mbarucu, Issa Hassani, Allan Ally, Kaisi Kaisi, Abdina Abdina, Allawi Msenga, Mohamed Mtutuma,  Salehe Ally, Abdi Hatibu, Bakari Malija, Abdallah Ally, Said Mohamed, Salimu Mwafi si, Saleh Rashid, Abdallah Said, Rehema Kawambwa, Salma Ndewa, Athumani Said, Dickson Leason na Nurdin Msati.

Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama za kufanya uhalifu, kufanya mkusanyiko usio halali na kufanya mgomo baada ya makatazo halali ya polisi.

Walikuwa wakidaiwa Januari 27, mwaka huu, maeneo ya wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kufanya uhalifu.

Pia mshitakiwa wa kwanza hadi wa 28, walikuwa wanadaiwa siku hiyo katika ofi si za CUF, karibu na Hospitali ya Temeke, bila halali walifanya mkusanyiko kwa nia ya kufanya maandamano yasiyo halali kwenda viwanja vya Mbagala Zakhem.

Shauri hilo lilikuwa katika hatua ya usikilizwaji, ambapo jana lilikuja kwa kutajwa na lilipangwa kuendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, Januari 5, mwakani.

No comments:

Post a Comment