Monday 11 January 2016

BALOZI KARUME AMSHUKIA FATMA KARUME, ASEMA DK. SHEIN RAIS HALALI WA ZANZIBAR


BALOZI mstaafu Ali Karume, amesema Rais Dk. Ali Mohamed Shein wa Zanzibar, anaendelea kushika wadhifa huo kihalali na kuwakosoa wote wanaohoji uhalali wa kuendelea kwake kuviongoza visiwa hivyo.
Aidha, amemjia juu mwanasheria Fatma Karume, aliyewahi kudai kwamba Dk. Shein hapaswi kuendelea kuongoza kwa kuwa muda wake wa uongozi umekoma.
Mbali na hilo, Fatma alidai kuwa kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar, uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, hakukutokana na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) bali ni uamuzi wa Mwenyekiti wa tume hiyo Jecha Salim Jecha.
Akizungumza katika kongamano la kumbukumbu ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Karume ambaye ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Mzee Abeid Amani Karume, alisema Dk. Shein anaongoza Zanzibar kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.
Balozi Karume alisema kwa sasa Dk. Shein ndiye rais halali wa Zanzibar hadi pale uchaguzi utakapofanyika na rais mwingine kuapishwa.
Akimzungumzia Fatma Karume, ambaye ni mtoto wa kaka yake, Rais mstaafu Amani Abeid Karume, alisema ana wasiwasi kwamba elimu yake si iliyoshiba na inayoweza kumfanya aone vitu kwa mtazamo sahihi wa kisheria.
Kwa mujibu wa Balozi Karume, hali hiyo huenda inachangiwa na kusoma kwenye vyuo visivyo na viwango vya kimataifa vyenye kupika wataalamu.
“Fatma hawezi na hana mamlaka ya kumwambia Dk. Shein akae pembeni kupisha rais mwingine. Yuko madarakani kwa mujibu wa sheria na ataendelea kuongoza nchi kulingana na katiba inavyotaka,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Mjini, Baraka Shamte, ambaye ni miongoni mwa wanasiasa wanaoyafahamu vyema Mapinduzi ya Zanzibar, akiwasilisha mada katika kongamano hilo, ikisema baadhi ya viongozi wa CCM wamechangia kuvuruga mambo kwa kushirikiana na wapinzani.
Alisema huu ni wakati kwa kila mzanzibar kutambua thamani ya mapinduzi hayo na kuhakikisha anayalinda ili kuepuka kurudi kwenye utawala wa kisultani.
Awali, akifungua kongamano hilo lililoandaliwa na Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu la CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar) Vuai Ali Vuai, aliwataka vijana kuwa mstari wa mbele kuyalinda mapinduzi hayo.
Vuai alisema Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964, yalitokana na vijana waliojitolea kwa mioyo yao yote ili kulinda utu wa mwafrika, hivyo ni vyema vijana wa sasa nao wakasimama imara kuhakikisha wanayalinda kwa nguvu za zote.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, alisema umoja huo upo tayari kusimama imara kuhakikisha mapinduzi matukufu yanalindwa kwa gharama yoyote.
“Vijana tupo tayari kuyalinda mapinduzi yetu kwa gharama yoyote. Tunatambua umuhimu wake katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa kwenye mikono salama,” alisema.
Kongamano hilo ni miongoni mwa shughuli zinazoendelea kwa ajili ya kumbukumbu ya mapinduzi hayo, ambazo kilele chake kitakuwa kesho katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Miongoni mwa shughuli hizo ni pamoja na matembezi ya vijana zaidi ya 700, ambayo leo yatapokelewa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Shein katika viwanja vya Maisara.

No comments:

Post a Comment