Monday 11 January 2016

SERIKALI KUWASAIDIA WALIOBOMOLEWA NA KUKOSA MAHALI A KWENDA

SERIKALI imesema inakusudia kuwasaidia watu wanaoendelea kuishi katika bonde la Mkwajuni, ambao nyumba zao zilibomolewa na hawana mahali pa kwenda.

Imesema itafanya sensa ya kujua ni watu wangapi ili iweze kuwabaini na kuona ni njia gani wataweza kuwasaidia watu, ambao wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo licha ya nyumba zao kubomolewa.

Hata hivyo, imesema itaendelea na bomoabomoa katika bonde la Mto Msimbazi, kwa utaratibu ambao hautaleta usumbufu kwa wananchi, kama ilivyokuwa awali kwa kuwa serikali haitaki chuki na wananchi.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba, wakati alipofanya ziara ya kutembelea shughuli ya usafishaji maeneo yaliyobomolewa katika bonde la Mkwajuni, Dar es Salaam.

Alisema sheria hairuhusu watu kujenga makazi kando ya mito au mabonde yanayopitisha maji, hivyo kinachofanyika ni utekelezaji wa sheria na sio jambo lingine lolote.

"Nimeona lakini serikali imeagiza ifanyike sensa na itakayosimamiwa na viongozi wa serikali ya mtaa wenu ili tupate taarifa sahihi na kuona namna ya kuwasaidia," aliwaambia baadhi ya wananchi wanaoendelea kuishi kwenye maeneo hayo kutokana na kutokuwa na pahala pa kwenda.

Alisema serikali haiwezi kuwaruhusu kuendelea kuishi eneo hilo kwa kuwa mazingira hayo ni hatarishi kwa maisha yao na ni kinyume cha Sheria ya Afya na Mazingira na ndio maana imechukua uamuzi wa kubomoa.

Waziri Makamba, alitoa siku saba kwa Mtendaji wa Kata ya Kigogo, Mzee Salum, kuhakikisha anawafahamisha wananchi kuhusu mpango wa kusafisha eneo hilo na athari za kuishi katika mazingira hayo.

Katika ziara hiyo, Waziri Makamba alikutana na mkazi mmoja Athumani Omari, ambaye alidai hana pa kwenda ingawa alikuwa anamiliki nyumba katika eneo hilo bila nyaraka yeyote.

Kauli hiyo ilimfanya Makamba kumwambia asubiri sensa hiyo ifanyike na ndio maana ameagiza ifanywe na viongozi wa mtaa na serikali itaona ni namna gani itaweza kuwasaidia.

No comments:

Post a Comment