Sunday 10 January 2016

BIL. 15.7/- ZASAMBAZWA AKAUNTI ZA SHULE


SERIKALI imesema sh. bilioni 15.7 zimesambazwa kwenye akaunti za shule ili kutekeleza ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya kutoa elimu bure kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne, mpango unaoanza mwaka huu.

Imesema fedha hizo zimepelekwa shule kupitia halmashauri zote nchini.

Mbali na hilo, imesema imekusanya sh.bilioni 18.77, ambapo kati ya fedha hizo, sh.bilioni tatu zimepelekwa kwenye vyombo vya usimamizi wa mitihani.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango,  alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, jukumu lililobaki ni kwa wakuu wa wilaya nawakurugenzi kufanya juhudi za kusimamia fedha hizo ili kutekeleza ahadi ya rais.

Dk.Mpango aliwaonya watakaotumia fedha hizo kinyume na lengo lililokusudiwa kuwa, watashughulikiwa kwa kutowajibika.

“Jambo linalofuata ni kuwataka wakuu wa shule hizo kuweka taarifa zao kwa uwazi kwenye ubao wa matangazo ili kila mtu aweze kuona kiasi gani kimetolewa kutoka serikalini,”alisema. 

Alisema kwa sasa wananchi wanapaswa kutoa taarifa za kufichua madudu yanayofanywa na watu watakaohujumu fedha hizo ili kuimarisha sekta ya elimu kwa kutoa fursa ya watoto wote kupata elimu.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kuongeza msukumo wa kukusanya kodi katika maeneo ya sekta ya utalii, tozo za misitu na uvuvi ili kupata mapato yanayostahili na kufanya maendeleo makubwa katika kipindi kifupi.

Dk.Mpango alisema hatua hiyo imetokana na mabadiliko makubwa yaliofanywa kwa kuwashughulikia watumishi wasiokuwa waaminifu katika ukusanyaji wa kodi na kuwabakisha waaminifu, ambao wanakusanya kodi stahiki kwa wafanyabiashara.

Hata hivyo, alisema serikali ipo kwenye mpango wa kutengeneza sheria ya ukusanyaji kodi za majengo, maarufu kwa jina la 'estate' ili kuongezea mapato.

Alisema kutokana na miji mingi kuendelea kukua, ni fursa pekee kwa serikali kukusanya kodi hizo kwa kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alisema hatua ya serikali kufanikiwa kupata fedha hizo, inatokana na jitihada za ukusanyaji kodi, ambapo kwa sasa TRA imevuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwezi Desemba, mwaka jana, ambapo imekusanya sh.trioni 1.4 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema serikali inaendelea na juhudi za kuziba mianya ya upotevu wa kodi na kwa sasa ipo kwenye hatua za mwisho za kuandaa sheria ya ukusanyaji wa majengo ya makazi (estate) na kwamba itasaidia kuhakikisha kodi zote hazitopotea.

Alisema kodi zote stahiki zitalipwa inapostaili na kwamba kwa namna moja ama nyingine, sheria husika zitatumika katika shughuli za ukusanyaji kodi.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Beno Ndulu alisema serikali ya awamu ya tano imeamua kuongeza juhudi za ukusanyaji wa kodi kinachohitajika kwa sasa ni kusitisha ununuzi wa bidhaa za kutoka nje ya nchi.

Profesa Ndulu alisema kuna haja ya kusitisha kuagiza na kununua vitu visivyo kuwa muhimu ili kutengemaa kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kwakufanya hivyo tabia ya kuomba misaada itakwisha na kuanza kujitegemea. 

No comments:

Post a Comment