Sunday 10 January 2016

PROFESA NDALICHAKO AICHARUKIA NECTA



SERIKALI imetoa siku saba kwa Menejimenti ya Baraza la Mitihani la Taifa Tanzania (NECTA), kueleza sababu za kitaalamu za kubadilisha baadhi ya mifumo ya uendeshaji katika taasisi hiyo.

Agizo hilo lilitolewa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Stadi, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye alisema mifumo hiyo ina maswali mengi kutoka kwa wadau wa elimu na kwamba utekelezaji wake haukuwa shirikishi.

Alisema kutokana na hali hiyo, NECTA inapaswa watoe maelezo kuhusu umuhimu wake na chanzo cha kuitumia kama haina tija kwa maendeleo ya elimu nchini.

Mifumo iliyobadilishwa na NECTA ni wa kutunuku ufaulu kwa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kutoka wa awali wa ujumla wa pointi (divisheni) na kutumia wa wastani wa pointi (GPA) pamoja na ule wa  kutoa mitihani miwili ya taifa kwa watahiniwa binafsi.

Profesa Ndalichako alisema serikali inahitaji maelezo ya kitaalamu kuhusu masuala hayo kwa sababu kiuhalisia, sababu zilizoainishwa kwake awali na Dk. Charles Msonda, ambaye ni Katibu Mtendaji wa NECTA, hazina mashiko.

Alisema NECTA ni taasisi muhimu kwa maendeleo ya taifa kupitia sekta ya elimu na haihitaji ujanja ujanja kwenye uendeshaji wake na kwamba, inahitaji weledi na ufanisi hasa linapokuja suala la kufanya maamuzi ya mifumo.

"Mifumo ya uendeshaji katika taasisi za serikali ikiwemo NECTA ina misingi yake inayotakiwa kuangaliwa kila mara linapokuja suala la kufanya maamuzi ya kimifumo.  Kwa mfano, hili mlilolibadilisha limetokana na azimio la Musoma la 1974 na limekiukwa," alisema.

Aidha, alisema ili kuendelea kuheshimika ndani na nje ya nchi, NECTA haina budi kusisitiza uwajibikaji wa watumishi wake, kusimamia misingi yake ya utendaji na kukataa kutumiwa au kushurutishwa na mtu au idara yeyote kuhusu maamuzi yake.

Akizungumza jana, jijini Dar es Salaam na menejimenti ya NECTA, Ndalichako  alisema aliwahi kuitumikia taasisi hiyo kwa miaka tisa kuanzia 2005, ambapo kwa kipindi hicho amejifunza mengi na kufanya mengi hivyo anaifahamu vizuri.

Alisema kwa nafasi aliyonayo sasa, anaendeleza dhana ya 'Hapa Kazi Tu', ambayo itajenga mfumo madhubuti kwenye sekta ya elimu nchini, itakayotoa elimu bora kwa mwanafunzi kulingana na kiwango chake cha elimu.

Alisema zama za wanafunzi kuchora mazombi kwenye karatasi za kujibia mtihani wa taifa au kuandika namba ya mtihani kisha kusubiri muda wa kutoka, zimepita na kwamba haiwezekani mwanafunzi asome miaka minne akakosa cha kuandika kwa saa tatu.

"Nakumbuka wachora mazombi kwenye karatasi ya mtihani, hii haikubaliki mwisho wao umefika. Wasahihishaji mnatakiwa muangalie na unapofika wakati wa kutoa majibu, iwekwe wazi matatizo yaliyojitokeza ili serikali tujue namna ya kudhibiti," alisema Ndalichako.

Ndalichako alikiri kuwepo kwa changamoto nyingi kwenye sekta ya elimu, lakini alisema kuwepo kwa umakini kwa watumishi wa sekta hiyo kutazitatua kwa kiasi kikubwa.

Alisema kitendo cha darasa la wanafunzi 40 kupata alama F wote kwenye mtihani wa taifa, hakikubaliki kwa sababu wana uelewa tofauti, hivyo lazima kuna tatizo mahali.

Awali, akimhoji Dk. Msonda kuhusu mabadiliko ya kimfumo yaliyofanyika kwenye taasisi hiyo, alisema alitaka kuelezwa kwa kina, lakini katibu mtendaji huyo alijibu kuwa bodi ya NECTA ilifanya mabadiliko hayo baada ya kupokea maelekezo ya wizara.

"Waziri sisi tulifanya hivi kwa kufuata maagizo ya wizara na sababu kuu ilikuwa ni kuweka mfumo mzuri wa uwiano kwenye ngazi na taasisi mbalimbali, ikiwemo TCU na sisi wa sekondari hasa linapokuja suala la kupanga vyuo.

"Utaratibu wa GPA unawarahisishia TCU kazi wanapowapangia wanafunzi vyuo (kudahili), haishushi viwango vya ufaulu kama wanavyodhani wengi," alisema Dk. Msonda.

Aidha, kuhusu swali la pili alilohojiwa na waziri kuhusu umuhimu wa kuwepo mitihani miwili kwa watahiniwa binafsi, alisema walifanya hivyo kutokana na malalamiko ya watahiniwa hao kuhusu kuonewa kwenye utungaji mitihani, ikilinganishwa na watahiniwa wa shule.

Profesa Ndalichako aliyakataa majibu hayo kwa kuwa mtihani wa pili unaofanywa na watahiniwa hao, unaitwa upimaji endelevu,  kitu ambacho ni upotoshwaji wa maana halisi ya upimaji endelevu.

"Upimaji endelevu ni pale mwanafunzi anapoangaliwa muda wote akiwa shuleni maendeleo yake kitaalumu, sasa hawa watahiniwa binafsi unapowapa huu mtihani umewapimaje? Unajua waliko? Kwa sababu mtu unakutana naye siku ya mtihani tu humjui, hakuna maana kwa kweli," alisema waziri.

Alimtaka Dk. Msonda kuliangalia suala hili haraka ili kama halina umuhimu mwaka huu, mtihani wa upimaji endelevu kwa watahiniwa binafsi usifanyike kwa sababu unaongeza gharama kwa serikali.

"Kufanyika mitihani miwili kunaongeza gharama kwa sababu wasahihishaji wanaongezeka na inabidi serikali iwatunze, kweli liangalieni hili, mtuletee sababu ya kuwepo kwake, tusifanye usanii kwenye mitihani," alisema.

Baada ya mahojiano hayo yaliyochukua takriban saa nzima, Dk. Msonda, alikiri kupokea maagizo ya waziri na kuahidi kuyatekeleza katika muda waliopewa, ambapo pia alisema mifumo inayotumika si ya kudumu, inaweza kubadilika muda wowote.

Alisema licha ya changamoto zilizopo, bado wanajitahidi kutekeleza majukumu yao bila kuchoka, ambapo sasa wanatumia teknolojia ya kisasa kutoa matokeo kwa watahiniwa ikiwemo njia ya simu ya kiganjani.

Pia, wanajitahidi kuhakikisha matokeo ya mitihani hayachelewi ili kutoa nafasi kwa wazazi, walezi na wanafunzi kujiandaa kwa ajili ya kuanza masomo katika mwaka mpya wa masomo.

"Tunafanya kazi usiku na mchana ili matokeo tuwe tunayatoa mapema, yaani wanafunzi wafungue shule huku wakiwa tayari wanajua matokeo yao kwa mitihani husika," alisema.

Kabla ya kikao hicho cha menejimenti, Waziri Ndalichako aliyeambatana na Katibu Mkuu, Maimuna Tarishi na Kamishna wa Elimu, Profesa Eustella Bhalalusesa, alizungumza na watumishi wote wa baraza ambao aliwaahidi kufanya nao kazi kwa karibu na kila mara atawatembelea kikazi.

No comments:

Post a Comment