Saturday 30 January 2016

DC MAKONDA AINGILIA KATI MGOGORO WA SUMAYE NA WANANCHI



WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameiangukia serikali na kuomba msaada baada ya wananchi kuchukua sheria mkononi na kuvamia eneo lake la ekari 33 lililopo Mabwepande, Dar es Salaam.

Aidha, serikali imemhikikishia kuwa haina mpango wa kumkandamiza mtu mnyonge wala tajiri, hivyo itahakikisha inatoa haki kwa kila mmoja baada ya wiki mbili kwa kuwa imesikiliza pande zote mbili katika mgogoro huo.

Akizungumza katika kikao cha pamoja kwenye Kijiji cha Kimondo, Mtaa wa Mji Mpya, Kata ya Mabwepande, jana, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, alisema ili kumaliza mgogoro huo ambao Sumaye ameiomba serikali kuingilia kati ni lazima busara itumike.

Makonda amezitaka pande zote mbili kuiachia serikali kwa wiki mbili ili kutafuta njia bora ya kumaliza tatizo hilo huku wananchi wakitakiwa kuacha kuendelea na ujenzi na kugawiana maeneo katika shamba hilo. Ì

Serikali ya Rais Dk. Magufuli ni sikivu na ndiyo maana ilikuwa tayari kumsikiliza Waziri Mkuu wetu mstaafu Sumaye na kusikiliza wananchi ili kutenda haki. Tunatambua migogoro ya ardhi ilivyokuwa na athari kwa jamii, hatuna mpango wa kumkandamiza tajiri wala mnyonge,îalisema Makonda.

Alisema katika eneo hilo anajua jinsi wananchi walivyotumia nguvu katika kuwekeza ujenzi na rasilimali zao, lakini kwa sasa wasitishe shughuli hizo na za kuendelea kugawana maeneo na Sumaye pia kuacha uwekezaji ili kutafuta suluhu.

Makonda alisema zipo njia nyingi zitakazotumika kumaliza mgogoro huo, ikiwemo kufuata sheria kwa kuangalia iwapo Sumaye alikiuka taratibu za kumiliki ardhi kama ilivyodaiwa na wananchi ili kuona hatua gani serikali ichukue.

Aliongeza kuwa:ìPia wanaweza kukaa na Sumaye na kuzungumza naye ili kukubali hasara kwa kutoa eneo kidogo na kuwapatia wananchi hao ambao hawana makazi au manispaa kutafuta eneo mbadala na kuwauzia kwa bei nafuu.

” Mkuu huyo wa wilaya, alizitaka pande hizo mbili kutambua umuhimu wa kulinda amani katika mgogoro huo na changamoto zilizopo kutatuliwa bila kutumia nguvu. Makonda pia ameiagiza serikali ya kijiji kufanya utambuzi wa wananchi hao wenye makazi katika shamba la Sumaye.

Awali, katika mkutano huo, Sumaye alimweleza Makonda jinsi serikali ilivyo na kazi ngumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi na kuomba kutumia busara zake kumpatia eneo hilo analomiliki kihalali.

ìMheshimiwa mkuu wa wilaya kama nilivyokueleza awali serikali yetu ina kazi ngumu sana hasa kutokana na viongozi wa chini kutokuwa wasikivu na wakweliÖ eneo hili nalimiliki kihalali, nina nyaraka zote na ninalipia kila mwaka na nilikuwa katika mpango wa kutafuta wafadhili ili kuliendeleza kwa kujenga chuo kikuu,îalisema.

Alisema yeye na familia yake waliuziwa eneo hilo tangu mwaka 1997 na anaamini serikali itatenda haki. Diwani wa kata hiyo, Suzan Masawe, alisema ana uthibitisho kuwa eneo hilo lilikuwa pori na Sumaye alilitelekeza kwa muda mrefu na kusababisha uhalifu ikiwemo wanawake kubakwa, mali za wizi kufi chwa na uhalifu mbalimbali.

Alisema kutokana na hatua hiyo, walimtafuta Sumaye lakini hakuwa na ushirikiano kwa kuwa hata alipofanya uwekezaji kwa kuchimba kisima cha maji alikataa kuwapa wananchi. Suzan alisema kutokana na hasira za wananchi hao kwa kukosa huduma za kijamii kwa muda mrefu ikiwemo eneo hilo kutokuwa na shule, zahanati wala kituo cha polisi waliamua kuvamia na kujigawia maeneo.

Mmoja wa wananchi hao, Athuman Mnubi, alikiri kweli hawana umiliki halali wa eneo hilo na katika hatua ya kutafuta makazi walivamia msitu huo uliotelekezwa na Sumaye. Alisema wanaamini kutokana na ahadi ya serikali ya Rais Dk. John Magufuli katika kuchukua maeneo yaliyotelekezwa na wawekezaji, watasaidiwa.

Wakati huo huo, Makonda alisimamisha msafara wake na kukamata baadhi ya malori ya kokoto na mchanga, wafanyakazi na mwekezaji wa kigeni kutoka India, Sules Waljan, wanaochimba mchanga, kokoto na kifusi katika eneo la Mabwepande.

Hatua hiyo ilitokana na kuona uharibifu mkubwa wa mazingira na alipowahoji wafanyakazi na mwekezaji huyo kama wana vibali, walisema hawana. 


Kutokana na hilo, aliwafi kisha watuhumiwa hao Kituo cha Polisi cha Wazo Hill ili kutoa maelezo ya kina na kusema serikali inaingia gharama kubwa kutokana na uharibifu huo wa mazingira ambao pia unafanywa katika vyanzo vya maji na matengenezo ya madaraja yanayoharibiwa ni makubwa.

No comments:

Post a Comment