Thursday 7 January 2016

OPARESHENI YA KUWATIMUA WAHAMIAJI HARAMU KUANZA LEO NCHI NZIMA

SERIKALI imetangaza kuanza kwa oparesheni kubwa ya kuwasaka wahamiaji haramu wanaoendesha shughuli zao nchini kinyume cha sheria, inayotarajiwa kuanza leo.

Aidha, serikali imetangaza kufuta vibali vyote vya muda vya wageni kuishi nchini, baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu mkubwa.

Oparesheni hiyo itawahusu wageni wanaofanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya  Nchi, Hamad Masauni, alisema oparesheni hiyo inafanyika kutokana na kuwepo kwa wageni wengi, ambao wanaishi nchini  na kuendesha shughuli ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.

Alisema hali hiyo inaathiri fursa za ajira kwa Watanzania, hasa wenye taaluma na ujuzi wa kuendesha biashara na kazi hizo.

“Pia oparesheni hiyo itawakumba wafanyakazi ambao wameajiriwa kama viongozi katika taasisi na mashirika kinyume cha sheria na ambao wamekuwa wakitumia vyeo vyao kuwanyanyasa wafanyakazi wazalendo kwa kuwadhalilisha, hivyo kukiuka tararibu na sheria,”alisema.

Masauni alifafanua kuwa oparesheni hiyo itakuwa kubwa katika kuwasaka na kuwakamata na kisha kuwafikisha kortini wahusika wote na kuwarudisha katika nchi zao.

“Wapo wafanyabishara na wafanyakazi wa kigeni ambao wanafanya kazi ambazo sio zile walizoomba kufanya.  Hawafuati sheria na taratibu za  nchi za uwekezaji. Tutawakamata na kuwashughulikia. Tunaomba waondoke haraka kabla ya kukumbwa na oparesheni hii,” alionya Masauni.

Alisema oparesheni hiyo haimaanishi Tanzania inawachukia raia wa kigeni, bali inalenga kuhakikisha sheria na taratibu za vibali vya kuishi nchini zinafuatwa.

Katika hatua nyingine,Masauni alisema serikali imefuta vibali vya muda vya kuishi nchini baada ya kubaini  wageni wengi wamefanya udanganyifu mkubwa.

Alisema wengi wa wageni waliokuwa wakiingia nchini kwa kutumia vibali vya muda, walikuwa wakifanya udanganyifu wa  kuvifanyia marekebisho ‘ku- renew’  kila wakati  na kufanya waishi nchini kwa muda mrefu wakitumia vibali hivyo vya muda.

“Badala yake tutatumia utaratibu wa vibali vipya. Najua kuna malalamiko mengi baada ya utaratibu wa awali kufutwa, lakini hatuna jinsi. Tutaendelea kutumia utaribu huu mpya ili kuepuka udanganyifu mkubwa uliokuwa unafanyika,”alibainisha.

Katika kudhibiti watendaji wa Idara ya Uhamiaji, wanaojihusha na vitendo vya rushwa na kutokuwa waadilifu, Masauni alisema hivi sasa idara hiyo imeingizwa kwenye mfumo wa kijeshi, hivyo  itaanzishwa mahakama ya  kijeshi ndani ya idara hiyo.

“Tunajua kuna baadhi ya watendaji wa idara ambao si waaminifu na walikuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa, ikiwemo kuchelewesha kwa makusudi wateja kupata pasi za kusafiria…mahakama hii itawashughulikia,” alisema Masauni.

Wakati huo huo, Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, imesema imeanza utekelezaji wa oparesheni ya kukamata wahamiaji haramu.

Akizungumza na waandishi wa habari, jana, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji (RIO), mkoani humo, John Msumule, alisema oparesheni hiyo iliyoanza jana, inalenga kukamata  wahamiaji zaidi ya 350, wanaofanya kazi kwenye kampuni, shule, serikali, taasisi za dini na nyumbani.

“Hatuwezi kukubali wageni kufanya kazi ambazo tayari Watanzania wana uwezo wa kuzifanya. Oparesheni hii itakwenda mkoa mzima na kuwakumba wale wote ambao wanaishi nchini bila vibali vya kufanyakazi ambazo Watanzania wanaweza kuzifanya,”  alisema.

Alitoa wito kwa waajiri na waajiriwa, ambao wanafanya kazi ambazo kimsingi ni za Watanzania au taaluma hizo, waondoke haraka kabla ya oparesheni hiyo haijawakumba.

“Kwa mwaka uliopita, kuanzia Januari Mosi  hadi Desemba 31, tulifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 182, kuwafikisha mahakamani na kuwatimua nchini raia wa  Ethiopia 211,” alisema.

Aliongeza kuwa pia waliwakamata Watanzania 15 waliokuwa wanajihusisha na  kuwahifadhi na kuwasafirisha wahamiaji haramu.

Kuhusu gharama za kuwasafirisha kurudi kwao wageni watakaokamatwa na ambao hawana uwezo wa kujigharamia, Msumule alisema serikali iko tayari kugharamia kwa sababu oparesheni hiyo inalenga kudumisha haki ya Watanzania katika taifa lao.

Alitoa rai kwa wananchi watakapowaona raia wa kigeni wanaowatilia shaka  kuwa wanaishi kinyume cha sheria, kutoa taarifa mara moja katika idara hiyo.

Hata hivyo, Msumule, alisema idara hiyo inakabiliwa na changamoto ya vitendea kazi, hasa magari ambayo licha ya uchache, mengi  ni mabovu na uhaba wa watendaji.

1 comment:

  1. Hapa ndio Magufuli ameanza kutumia jina lala "Pombe" ni Upusi mtupu. ni watanzania wangapi wako inchi zingine kama Kenya na wanafanya biashara

    ReplyDelete