Thursday 7 January 2016

TAKUKURU YAANZA KUICHUNGUZA TAZARA




WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amesema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeanza kufanya uchunguzi ili kubaini ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA).
Profesa Mbarawa alisema hayo jana, Dar es Salaam, alipokuwa alitoa mwelekeo wa utendaji wa shirika hilo kwa watendaji na watumishi wa TAZARA.
Alisema serikali ya awamu ya tano inalitaka shirika hilo kufanya kazi kibiashara kwa kuhudumia wasafiri na wasafirishaji kikamilifu ili kuinua uchumi wa shirika hilo na kuliondolea unyonge na migogoro ya mara kwa mara.
Kuhusu ubadhirifu unaotokea TAZARA, Profesa Mbarawa alisema tayari uchunguzi unaofanywa na TAKUKURU umeanza na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahalifu wote bila kujali wanatoka upande gani wa TAZARA.
Aliwataka watendaji na wafanyakazi wa shirika hilo kufanyakazi kwa umoja, uwazi na uadilifu ili kufikia malengo yaliokusudiwa na kuhuisha ustawi wa shirika.
“Acheni  kufanyakazi kwa upendeleo na usiri kwani huo ndio mwanzo wa hujuma na ubadhirifu, hali inayochochea malalamiko na kudumaza TAZARA,” alisema.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa TAZARA, Betram Kiswaga, alisema shirika hilo linakabiliwa na changamoto za kimtaji, kiufundi na upungufu wa injini na mabehewa, hivyo ameiomba serikali kuiwezesha ili imudu kujiendesha.
Alisema tayari shirika hilo limeanza kupata wasafirishaji wa uhakika, hivyo kuimarika kimtaji kutavutia wasafirishaji wengi zaidi.

No comments:

Post a Comment