Thursday 7 January 2016

SERIKALI YAPINGA NAULI ZA DART




WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali haijaridhia viwango vipya vya nauli ya mabasi yaendayo kasi vilivyopendekezwa na waendeshaji wa huduma ya mabasi yaendayo kasi Dar es salaam (UDART).
Amesema gharama hizo ni kubwa mno kwa wananchi na watumishi na kwamba mradi huo, ulilenga kumrahisishia mtumishi wa serikali anayeishi nje ya jiji.
“Serikali iliwekeza katika mradi huu ili kusaidia watumishi na wananchi ambao hawana vipato vikubwa,” amesema Waziri Mkuu.
Majaliwa alisema hayo jana, alipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea mkoani Ruvuma, alikokwenda kwa ziara ya siku tatu.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya DART, nauli ya kutoka Mbezi hadi Kimara sh. 700, Mbezi hadi Kariakoo sh. 1,200 na nauli ya kutoka Mbezi hadi Mwenge sh. 1400 wakati wanafunzi watatozwa nusu ya viwango hivyo vya nauli.
Waziri Mkuu alisema endapo UDA-RT itashindwa kutoa huduma ya usafiri huo kwa kuzingatia maisha halisi ya Mtanzania, serikali itauchukua na kuuendesha.
Aidha, ameagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi, na Mawasiliano pamoja na wadau, wakutane kupanga upya viwango hivyo na kama watashindwa serikali itaendesha mradi huo.
Novemba 25, 2015, Waziri Mkuu alimuagiza aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya TAMISEMI na waendeshaji wa mradi huo kupitia misuada yote na kurekebisha miundombinu ili mradi huo uanze kufanyakazi ifikapo Januari 10, mwaka huu.
Imebainika kuwa UDART hawakuandaa mpango wa biashara wala kuanisha gharama za uendeshaji.
Aidha, imebainika kuwa licha ya kampuni hiyo kutokuwa na mpango wa biashara na uwekezaji, vigezo vya nauli ilivyoviwasilisha kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA) havina uhalisia.
Majaliwa alisema lengo la kuanzisha  mradi huo wa usafiri ilikuwa  kutoa huduma kwa kuwapunguzia kadhia  wananchi pamoja na watumishi wa sekta mbalimbali, kutumia gharama kubwa kufika kwenye maeneo yao ya kazi.
“Kama mtumishi wa ngazi ya nchini anayelipwa mshahara wa sh. 260,000 kwa viwango vya nauli vilivyopangwa, atalazimika kutumia robo tatu ya mshahara wake kwenye nauli.
“Lazima ifahamike kuwa, mradi huu umeanzishwa kumuhudumia mwananchi, hivyo serikali haitosita kuuchukua na kuuendesha kama  wakishindwa kuweka nauli kwa mujibu wa gharama za uwekezaji na uendeshaji,” alisisitiza Majaliwa.
Alisema,  serikali haiwezi kuruhusu viwango hivyo vya nauli kutumika kwa sababu vitamuongezea mzigo mwananchi wa kulipa gharama kubwa zaidi kuliko uhalisia wa vipato vyao.
Hivyo aliagiza mradi huo haupaswi kuanza hadi viwango vya nauli vitakapoangaliwa upya kwa kuzingatia nauli zitakazomwezesha mwananchi kuzimudu.

No comments:

Post a Comment