Thursday 7 January 2016

VIGOGO TISA WASIMAMISHWA KAZI KIGOMA




KATIBU Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi John Ndunguru, amewasimamisha kazi watumishi tisa wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, kwa ubadhirifu wa fedha za umma.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, mjini hapa, Mhandisi Ndunguru, alisema kusimamishwa kazi kwa watumishi hao, kumetokana na tuhuma za ubadhirifu wa mali za umma.
Alisema tuhuma hizo zilibainika wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa, aliyoifanya hivi karibuni mkoani hapa.
Mhandisi Ndunguru alisema mkoa uliunda kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma hizo na kubaini kuwa, watumishi hao wamefanya udanganyifu katika mikataba mbalimbali na kuisababishia serikali hasara.
Alisema ubadhirifu uliofanywa na watumishi hao ni manunuzi hewa ya shajara yenye thamani ya sh. milioni nne, vipuri milioni nane pamoja na matumizi mabovu ya fedha za serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Alitaja ubadhirifu mwingine waliofanya watumishi hao ni kuuza majengo ya Kigodeco na Mibox kwa bei ya chini, ambayo ni sh. milioni 370, badala ya sh. milioni 470.
"Kamati imefanya kazi nzuri ya uchunguzi wa awali, hivyo kuanzia sasa namsimamisha kazi Willyfred Mwita, ambaye ni Ofisa Mipango, Emanuel Mkwe, ambaye ni mwanasheris, Boniface William, ambaye ni Mhandisi na Mussa Igugu, Ofisa Biashara.
Wengine ni Elimboto Zakaria, ambaye ni Mkaguzi wa Ndani, Leonard Nzilailunde, ambaye ni Ofisa Misitu, Shida Tadei, ambaye ni Ofisa Ugani, Bawili Mkoko, ambaye ni  Mhasibu na Omary Lubibi, Fundi Mkuu wa Magari.
Ndunguru alisema amewasimamisha kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi dhidi yao uendelee kufanyika kwa kina na maofisa kutoka TAMISEMI, ambao watawasili mkoani humo kwa ajili ya kazi hiyo.
Aidha, amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuhakikisha mali zote za serikali zilizouzwa kinyume na taratibu za kisheria, zinarudi kwenye halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment