Friday, 26 February 2016

MAWAZIRI WA MAGUFULI WAWEKWA MTEGONI, MAJALIWA AKABIDHIWA ORODHA YA WASIOJAZA FOMU ZA MAADILI


WAZIRI Mkuu, Kasimu Majaliwa amekabidhiwa majina ya mawaziri na manaibu mawaziri ambao hawajajaza fomu za maadili ya viongozi wa umma.

Majaliwa, alikabidhiwa majina hayo jana na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda, wakati wa hafla ya mafunzo yanayohusu maadili ya viongozi.

Mafunzo hayo yalifanyika Ikulu mjini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mawaziri na naibu waziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, Majaliwa alisema serikali inaridhishwa na utendaji wa kazi unaofanywa na mawaziri na naibu waziri katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Jaji Salome alisema sheria ya maadili ya viongozi wa umma ina majukumu kadhaa, ikiwa ni pamoja na kumtaka kiongozi wa umma kutoa tamko la rasilimali, maslahi na madeni na pia kutotumia vibaya rasilimali za umma.

Jaji Salome alisema sheria hiyo pia inamtaka kiongozi kujizuia na migongano ya maslahi, kutojilimbikizia mali na kutumia madaraka yake vibaya.

Alisema jambo hilo kisheria ni muhimu, lakini baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri hawajajaza fomu hiyo pamoja na hati ya uadilifu.

“Mheshimiwa kwa ruksa yako napenda nikukabidhi majina ya mawaziri na naibu mawaziri ambao hawajajaza fomu hiyo,” alisema.

Alisema hati ya uadilifu ilijazwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Rais Dk. John  Magufuli, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Jaji Salome alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo viongozi hao kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia maadili ya viongozi wa umma.

Alisema walipata taarifa nyingi za ukiukwaji wa maadili kwa viongozi na mgongano wa maslahi katika awamu iliyopita,  ambapo iliwahi kutokea waziri alimuagiza katibu mkuu amtengee fedha kwa ajili yake kwa kuwa ni waziri binafsi na akimuuliza nitatoa wapi, anamwambia utajua mwenyewe.

Hata hivyo, alisema sekretarieti imepewa mamlaka ikiwa ni pamoja na kupokea na kusikiliza malalamiko kuhusu kiongozi yoyote wa umma, yawe ya mdomo ama maandishi.

Alitaja mamlaka mengine ya sekretarieti hiyo kuwa ni kuanzia na kufanya uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa katika sheria na kukagua akaunti ya benki ya kiongozi pale ambapo wanatarajia kufanya uchunguzi kuhusu akaunti ya kiongozi husika.

Jaji Salome alisema kimsingi maadili yamelenga kuzuia mgongano wa maslahi, upendeleo, matumizi mabaya ya taarifa za ofisi na mwenendo usiofaa kwa kiongozi wa umma ili kuimarisha na kuendeleza dhana za uadilifu, uwajibikaji na uwazi.

Kwa upande wake, Majaliwa alisema serikali inaridhishwa na kazi zinazofanywa na mawaziri katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Alisema serikali ina dhamira ya kweli ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi na kwamba, tayari imeanza kuchukua hatua na itaendelea kuchukua hatua hadi itakapojiridhisha kama mambo yanakwenda sawa.

Majaliwa alisema ni ukweli kwamba wananchi wanachukia rushwa na ufisadi na wamechoshwa na vitendo hivyo, kwani vinawanyima haki zao na kuitia hasara serikali, kutokana na mamilioni ya fedha ambayo yangeweza kutumika kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kupotea.

Aliwataka viongozi wa umma na sekta binafsi kila mmoja kwa nafasi yake, atimize ahadi zake kwa kuzingatia maadili ya viongozi wa umma.
Majaliwa aliwataka mawaziri na manaibu waziri kuzingatia sheria ya maadili kwa viongozi wa utumishi wa umma, kwani maadili ni nyenzo  kubwa katika kuleta maendeleo ya nchi.
“Chimbuko la maadili ya utumishi wa umma, lilianza tangu siku nyingi na yamekuwa yakitajwa katika sehemu mbalimbali, ikiwemo katika katiba ya nchi ya mwaka 1977, Sheria za Utumishi wa Umma na Kanuni za Utumishi wa Umma,” alisema.
Hata hivyo, alisema mafunzo hayo si semina elekezi kwa viongozi hao kama inavyojadiliwa katika mitandao ya kijamii, bali ni mafunzo ambayo yanalenga kutoa mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma na utekelezaji wa hati ya ahadi ya uadilifu na mada katika semina hiyo zitahusu masuala ya maadili tu.

No comments:

Post a Comment