Friday 26 February 2016

SERIKALI YAWAONYA WAFANYABIASHARA WANAOFICHA SUKARI




SERIKALI imesema kama kuna uhaba wa sukari nchini, utakuwa umesababishwa na watu wachache wanaohujumu uchumi wa nchi na watakobainika watanyanganywa vibali.

Aidha, imesema itahakikisha bei ya sukari inashuka ili iendane na uhalisia wa maisha  ya wananchi, wakiwemo wa kipato cha chini.

Mbali na hilo, imewataka anayefahamu ilipofichwa sukari, atoe taarifa kwenye mamlaka husika ili waliofanya vitendo hivyo wafutiwe vibali.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charlse Mwijage, alisema hayo jana Ikulu, mjini Dar es Salaam na kuongeza kuwa, siku Rais Dk. John Magufuli alipopiga marufuku uagizwaji wa sukari kutoka nje, sukari ilikuwepo ya kutosha.

“Kabla Rais hajatoa tamko lile kulikuwa na meli zinateremsha sukari, kwenye maghala ilikuwepo, sasa kama hivi haipo huo utakuwa uhujumu wa uchumi,” alisema.

Aliwataka wananchi wenye taarifa za watu wanaoficha sukari, kuwaripoti kwenye mamlaka husika ili wachukuliwe hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kunyanganywa leseni.

Mwijage aliwataka Watanzania kutokuwa na hofu kuwa sukari inaweza kupotea na kwamba, atahakikisha bei ya sukari inashuka ili iendane na maisha ya wananchi.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi wanaletewa sukari yenye ubora inayoendana na vipato vyao.

Kwa mujibu wa waziri huyo, baadhi ya wafanyabiashara walikuwa wakinunua kilo ya sukari kwa sh. 600 na wao walikuwa wakiiuza kwa sh. 2,000.

Alisema kuanzia sasa, wanafikiria kutoa bei elekezi ya sukari kama ilivyo kwenye nishati ya mafuta kwani hivi sasa hakuna bei elekezi ya sukari.


No comments:

Post a Comment