VIGOGO watatu wa Mradi wa
Mabasi yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam (DART) akiwemo Mtendaji Mkuu,
Asteria Mlambo, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Kiongozi huyo na watendaji
wenzake wawili na mfanyabiashara Yuda Mwakatobe, walifikishwa mahakamani hapo
jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwa tuhuma za kuisababishia
hasara serikali ya sh. milioni 83.5.
Mbali na Asteria, vigogo
wengine wa DART ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Evodius Katale na
Mwanasheria Mkuu, Francis Kugesha.
Asteria, Katale, Kugesha na
Mwakatobe walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious
Mwijage na kusomewa mashitaka matatu na Wakili wa Serikali, Jacqline Nyantori,
akishirikiana na Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson na mawakili kutoka
TAKUKURU, Vera Ndewoya na Stella Mafuru.
Akiwasomea mashitaka,
Jacqline alidai shitaka la kwanza linawakabili Asteria, Katale na Kugesha,
ambao wanadaiwa kuisababishia DART hasara ya sh. 83,564,367.
Alidai washitakiwa hao
walitenda kosa hilo, kati ya Septemba Mosi na Oktoba 31, 2013, Kinondoni, Dar
es Salaam, ambapo wakiwa na nyadhifa hizo, walishindwa kutekeleza majukumu yao
kwa weledi, hivyo kuisababishia DART hasara ya kiasi hicho.
Shitaka la pili na tatu
yanamkabili Mwakatore, ambaye anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), juu ya taarifa za fedha, hivyo kutozwa kodi
chini ya kiwango anachotakiwa kulipa.
Inadaiwa Juni 29, 2005,
katika ofisi za kodi za mkoa wa Ilala, Mwakatobe alitoa taarifa za uongo kwa
maofisa wa TRA, wakati akiwasilisha taarifa za kampuni yake ya Yukan Business
C. Ltd za mwaka wa fedha wa 2004, ambazo zilikuwa zina maelezo ya uongo, hivyo
kuwafanya maofisa hao kumtoza kodi chini ya ile aliyotakiwa kutozwa.
Mshitakiwa huyo pia
anadaiwa kutenda kosa kama hilo Mei 26, 2006, alipowasilisha taarifa za kampuni
hiyo za mwaka wa fedha 2005.
Washitakiwa hao, ambao
wanatetewa na Wakili Yuda Tadei, walikana mashitaka, ambapo upande wa jamhuri
ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba hauna pingamizi juu ya dhamana.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri
ulitoa angalizo kwa mahakama wakati unatoa masharti ya dhamana kwa washitakiwa
Asteria, Katale na Kugesha, izingatie kifungu cha 36(3)(e) na cha 5 cha Sheria
ya Uhujumu Uchumi juu ya kiwango kilichoko katika hati ya mashitaka.
Wakili Jacquline alidai
kutokana na matakwa ya sheria, washitakiwa hao watatu wanatakiwa kuwasilisha
mahakamani fedha sh. milioni 13.9 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani
hiyo.
Kwa upande wa wakili wa
utetezi, aliiomba mahakama kutoa masharti nafuu kwa kuzingatia kwamba,
washitakiwa ni maofisa wa serikali ambao hawategemewi kuruka dhamana.
Baada ya kuelezwa hayo,
hakimu aliwahoji washitakiwa iwapo wana hati za mali zisizohamishika, ambapo
Kugesha alidai wameletwa mahakamani wakitokea ofisini huku Asteria akidai ana
hati ya nyumba ipo nyumbani.
Hakimu Mwijage alitoa
masharti ya dhamana ambapo aliwataka washitakiwa Asteria, Katale na Kugesha,
kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja atakayetia saini dhamana ya sh. milioni 15 na
awe na barua ya utambulisho kutoka ofisi ya serikali, taasisi yoyote au kampuni
inayosajiliwa kisheria.
Pia, washitakiwa hao
wanatakiwa kuwasilisha mahakamani hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sio
chini ya sh. milioni 14, ambapo sharti hilo halitatimizwa kwa jana, lakini haliwezi
kuzuia wasipewe dhamana. Hata hivyo, walitakiwa kuzileta baada ya siku saba.
Kwa upande wa mshitakiwa wa
nne, alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja atatayetia saini dhamana ya sh.milioni
tano na awe na barua ya utambulisho kutoka ofisi yoyote ya serikali au taasisi
na kampuni iliyosajiliwa kisheria.
Washitakiwa Asteria, Katale
na Kugesha walitimiza masharti ya dhamana kwa kuwasilisha wadhamini.
Sharti la kuwasilisha hati
ya mali isiyohamishika liliweza kutimizwa na Kugesha, ambaye aliwasilisha hati
ya nyumba yenye thamani ya sh. milioni 299, huku Asteria na Katale wakipewa
muda hadi Machi 3, mwaka huu, kuwasilisha hati za mali zisizohamishika na
wakishindwa kufanya hivyo watafutiwa dhamana.
Hakimu Mwijage aliahirisha
shauri hilo hadi Machi 9, mwaka huu, kwa kutajwa.
No comments:
Post a Comment