Friday 26 February 2016

UTAFITI WA TWAWEZA WAONYESHA ASILIMIA 88 YA WATANZANIA WANA IMANI NA ELIMU BURE




ASILIMIA  88 ya wananchi wa Tanzania wanaamini kuwa ahadi  ya elimu bure itatekelezwa katika muda uliopangwa, jambo linaloonyesha  kuwa  wananchi  wana imani na ahadi hiyo.
Ripoti ya utafiti  uliofanywa na asasi isiyo ya kiserikali ya Twaweza ni sisi, iliyotolewa jana, Dar es Salaam, imebainisha kuwa asilimia 76, ya wananchi hao pia wanaamini  kuwa  elimu bure  itakuwa bora zaidi.
Wakati ripoti hiyo ikisema hayo, wasomi na wanasiasa wametoa maoni  yao kuhusu sera hiyo, wakimtaka Rais Dk. John Magufuli,  kuendelea kubuni njia zaidi za kuiboresha, ikiwa ni pamoja na kumaliza changamoto zinazotishia kuathiri utekelezaji wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo,  Aidan Eyakuze, alisema pamoja na  wananchi  wengi  kuwa na mtazamo  chanya, asilimia 15 wanaamini elimu  ya bure haitaboresha  elimu, kutokana na ongezeko kubwa  la uandikishaji  wa wanafunzi ambao  utatumia rasilimiali nyingi.
Eyakuze, alisema matokeo hayo yametolewa na Twaweza  kwenye muhtasari  wa utafiti wake wenye jina la ‘Mwanga Mpya’, kupitia maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko  kwenye sekta ya elimu’.
“Muhtasari huu  umetokana na takwimu  za sauti za wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye  uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi.

“Ripoti hiyo inatokana na takwimu zilizokusanywa kati ya Desemba 10, mwaka jana na Januari 2, mwaka huu,  kutoka kwa watu 1,894, wa Tanzania Bara  bila kuhusisha Zanzibar,”alisema Eyakuze.
Alisema utoaji wa elimu bure pamoja na  kukomesha michango shuleni,  kulikuja  katika wakati muafaka, ambapo  wazazi  wengi  walikuwa wanaelemewa na michango  shuleni.
Alisema kwa ujumla, asilimia 89 ya wazazi  wanakiri  kulipa  michango shuleni,  asilimia 80, wakiripoti kulipa  mpaka sh. 50,000 kwa mwaka, huku asilimia  nane wakilipa  zaidi ya sh.100,000 kwa mwaka.
Eyakuze alisema  matokeo hayo pia yamebaini kuwa, asilimia  49, wanaamini kwamba michango  yao  haitumiki ipasavyo  na asilimia  58 walisema michango  hiyo haijaidhinishwa  na serikali, ambapo asilimia 89 walisema walimu hutumia  michango hiyo  kujiongezea kipato.
“Kwa mujibu wa wazazi,   asilimia 66  ya michango hiyo  walidai hutumika  kulipa ulinzi , asilimia 57  mitihani ya majaribio, asilimia  34 madawati,  huku  kiwango  kidogo  kikielekezwa kwenye mahafari ambayo ni asilimia nne na safari za shule asilimia nne, ”alisema.
Utafiti  huo  pia ulionyesha kuwa, ruzuku  inayopelekwa  moja kwa moja shuleni,  ambayo ndiyo chanzo  kikuu  cha fedha  kwa shule , inaweza  isitoshe  kuziba pengo  la michango  iliyoondolewa.
“Asilimia  40 walisema ruzuku inayotolewa   huelekezwa  kwenye vitabu na nyenzo za  kujifunzia  , asilimia 20 vifaa vya kuandikia, asilimia 10  utawala  na asilimia 10  karatasi  za mitihani  na uchapaji,”alieleza Eyakuze.
Alishauri  kuwa  shule zinapaswa kuwa makini  na kiwango  kidogo cha fedha  kinachopatikana, kwani vitu vingi  ambavyo wazazi  huchangia  havijajumuishwa kwenye ruzuku.
“Pamoja na wananchi kuwa na imani  na ahadi ya elimu bure, wengi  wamekuwa na mtazamo tofauti juu ya ubora wa elimu  ya msingi  kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita,”alisema.
Alieleza kuwa, utafiti huo ulibaini kuwa  asilimia 49 ya wananchi  walisema  ubora wa elimu umeongezeka,  lakini asilimia  36 walisema elimu  imezorota na asilimia 14 walisema  hakuna mabadiliko yoyote.
“Asilimia 37 ya wananchi wanaamini kuna uhusiano  wa karibu  kati ya  jitihada  za mwalimu na matokeo  ya  darasa la saba. Vilevile   asilimia 93 wanaamini kuwa walimu  ndiyo  msingi wa maendeleo, asilimia 85 wanaamini  kwamba walimu wanaheshimika, asilimia  79 walimu  wanajivunia taaluma yao  na asilimia 60 walidai walimu wanapewa motisha  kuhakikisha watoto wanajifunza,”alieleza.
Alisema pamoja na hayo, asilimia 80 ya  wananchi  wanaamini  kwamba  walimu  hufanya kazi yao kwa ajili ya kujipatia kipato.
“Asilimia 52 walikubali kuwa  walimu wanalipwa vizuri kumudu maisha yao,  huku asilimia 42 wakisema hapana.Na kwenye suala la mazingira ya kufundishia  kama yanampa motisha  mwalimu, asilimia 58 walisema ndiyo  huku asilimia  34 wakisema hapana.  Asilimia  56 ya wananchi wanaamini  mishahara ya walimu   inaongezwa na asilimia  19 wanaamini mazingira ya kufundishia  yakiboreshwa vitaongeza ari ya kufundisha,”alieleza Eyakuze.
Alisema wananchi wameishauri serikali  kuboresha elimu, asilimia 82 wametaja masuala  yanayohusiana na walimu, asilimia  40 wametaja ufuatiliaji  wa karibu wa walimu  na asilimia  19 wameshauri kuongezwa mishahara.
“Asilimia 10 wameshauri kuongeza idadi ya walimu, asilimia saba kuongeza  vifaa vya kufundishia, asilimia nne kuongeza  mishahara na kulipwa kwa wakati,  asilimia mbili  walishauri walimu wapatiwe  nyumba  za kuishi  kama suluhisho,” alibainisha Eyakuze.
Katika hatua nyingine , wasomi na wasanasiasa nchini wametoa maoni  yao kuhusu sera hiyo, wakimtaka Rais Dk. Magufuli  kuendelea kubuni njia zaidi za kuiboresha, ikiwa ni pamoja na kumaliza changamoto zinazotishia kuathiri utekelezaji wake.
Mbunge wa  Nzega, Tabora, Hussein Bashe, alishauri  serikali kuunda tume maalumu ya kushughulikia changamoto za elimu, itakayotoa majibu ya changamoto zilizopo na kwamba, ikiwa hali itaendelea kuwa hivyo,  Tanzania itabakia kuwa katika janga kubwa la elimu.
“Pamoja na elimu kutolewa bure, lakini ni lazima tuzingatie ubora wa elimu hiyo. Tuache kupima ubora wa elimu  yetu kwa idadi ya watoto wanaoandikishwa, kisha kuwachuja kwa  kufeli au kufaulu mitihani. Naomba turudi katika meza ya pamoja  kujadili janga hili. Tukubali kwamba hili ni janga,” alisema Bashe.
Kwa upande wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Jovita Katabaro, alisema kuna umuhimu mkubwa wa watalaamu wa elimu nchini kuibuka na kutoa ushauri wa kukabiliana na changamoto zinazoibuka.
“Ni lazima tukubali kwamba kuna sehemu tulikosea, hivyo  turudi katika meza ya pamoja kujadili. Tuangalie tunatumia falsafa gani ya elimu, “alisema.
Kwa upande wake, Profesa Kitilya Mkumbo, alisema  jitihada kubwa zinahitajika ili kuboresha sekta ya elimu hapa nchini  zaidi ya serikali kufuta michango.

No comments:

Post a Comment