Sunday, 6 March 2016

SERIKALI YAWAONYA WATUMISHI WA AFYA

SERIKALI  imesema haitavumilia matukio yatakayofanywa na watumishi wa sekta ya afya, ambao watakwenda kinyume na matakwa ya maadili na taaluma zao katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Imesema haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kudhibiti hali hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipokuwa akizungumzia maadili ya utoaji wa huduma za afya nchini.

Alisema ameshaelekeza vyombo vya kusimamia maadili ya watoa huduma za afya nchini, likiwemo Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC), kuchukua hatua mara moja juu ya watoa huduma wote wanaotuhumiwa.

Ummy alisema watuhumiwa hao, wakiwemo wa Mtwara, Temeke na Nyamagana, iwapo tuhuma dhidi yao zitathibitika, hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kufutiwa usajili au leseni zao.

“Ni muhimu pia nikakumbusha kwamba kazi hii ya usimamizi wa maadili katika vituo vya kazi itafanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja wa wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala pamoja na wakurugenzi katika kuwasimamia, kuwaelekeza na kutambua mapungufu yaliyopo na kuchukua hatua zinazostahili.Tufanye kazi kwa pamoja ili kutekeleza kaulimbiu ya Rais Dk. John Magufuli inayosema ‘Hapa Kazi Tu,”alisema.

Alisema mtoa huduma wa afya anapaswa kuyajua, kuonya na kusahihisha mapungufu yanayotokea katika sehemu yake ya kazi na pia anatakiwa kuzingatia kiapo cha taaluma yake katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi ya kila siku.

Waziri huyo aliwaasa na kuwaagiza watoa huduma wa afya wote nchini, kufanya kazi zao kwa bidii na kwa kuzingatia weledi na maadili ya kitaaluma kama inavyoelekezwa.

“Ninasikitishwa sana na tabia ya watumishi wachache ambao wanafanyakazi kinyume na maadili ya taaluma zao. Tumezisikia wote taarifa mbaya kutoka Geita, Mtwara, Nyamagana, Temeke na kwingineko, ambazo wagonjwa au ndugu wa wagonjwa wamekuwa wakihudumiwa vibaya,”alisema.

Ummy alisema katika utoaji wa huduma za afya, yapo maadili ambayo mtoaji huduma anapaswa kuyajua na kuyazingatia, ikiwemo kuongea na mgonjwa au ndugu wa mgonjwa kwa lugha ya upole, yenye maelekezo na faraja.

Pia, alisema anapaswa kuepuka maneno makali kwa mgonjwa, kutomshika mgonjwa mwili wake bila ridhaa yake, uaminifu na mtoa huduma kumheshimu mgonjwa na kumsikiliza kwa makini pale anapomueleza tatizo lake.

Aidha, ameagiza mtoa huduma asimtoze mgonjwa gharama zisizostahili na kama kuna gharama zozote, zilipwe sehemu husika ya kupokelea fedha na asiongeze gharama za matibabu tofauti na ile iliyotajwa kwenye miongozo husika.

Kwa mujibu wa Ummy, Tanzania inazo sera, taratibu, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali, ambayo wamejiwekea ili kuhakikisha haki hiyo inapatikana kwa Watanzania wote katika utoaji wa huduma ya afya nchini.

Alisema vipo vituo 7,247 vya umma na binafsi katika ngazi mbalimbali, vyenye kuhudumiwa na wataalamu wa afya wa kada na ngazi tofauti.

Aliwapongeza watoa huduma wote ambao wanafanya kazi zao kwa ufanisi, upendo na uadilifu.

“Wengi wanatumia muda wa ziada kuendelea kuwahudumia wagonjwa hadi wanapoona wapo salama. Napenda kuwashukuru na kuwatia moyo waendelee kuwa na tabia hiyo nzuri kwa maslahi ya taifa letu,”alisema.

Juzi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, alimshusha madaraka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana, Nangi William na kumsimamisha kazi Muuguzi Mkuu, Suzan Lumash, kufuatia sakata la watoto  mapacha waliofariki dunia muda mfupi baada ya kuzaliwa hospitalini hapo.

Hata hivyo, baadaye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alimfukuza kazi Suzan na kusema  kwamba, wahusika watafunguliwa kesi ya mauaji na serikali haitawavumilia watumishi wa aina hiyo.

Kufuatia sakata hilo, madaktari na wauguzi waliotumbuliwa majipu hospitalini hapo wamefikia wanane, ambao ni Ngusa Masanja, Dk.Noorne Jandwa, Dk. Emeriana Mvungo na wauguzi ni Suzan Sindano, Maria Mkankule, Bibiana Moshi na Janeth Foya.

No comments:

Post a Comment