Sunday, 6 March 2016

DK. SHEIN ACHACHAMAA ULIPUAJI WA MASKANI YA CCM KISONGE



NA MWANDISHI MAALUMU, ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, amewataka wanachama na wapenzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wawe na subira na wasikubali kuchokozeka, kufuatia vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi yao na mali za Chama.

Dk. Shein, ambaye  ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), alisema hayo jana, baada ya kutembelea maskani ya Mwembekisongo, iliyoko Michenzani mjini Unguja, iliyoharibiwa
kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea Alhamisi iliyopita.

Kwa mujibu wa Katibu wa maskani hiyo, Mzee Yunus, mlipuko huo ulitokea kati ya saa sita kamili usiku na saa 6.30 usiku na kusababisha hasara kwa kuharibu ofisi na baadhi ya vifaa vilivyokuwemo.

“CCM tunatii sheria za nchi, lakini Jeshi la Polisi lazima litimize wajibu wake kwa kuwatafuta waliofanya kitendo hiki na kuwapeleka katika vyombo vya sheria,” Dk. Shein aliwaambia wananchi na viongozi waliokuwepo katika eneo hilo.

Dk. Shein alilitaka Jeshi la Polisi Zanzibar kufanya uchunguzi wa haraka na kuwabaini waliohusika na kitendo hicho na kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria mara moja.

Aliahidi kuisaidia maskani hiyo kufanya ukarabati wa sehemu iliyoharibika ili shughuli za maskani ziweze kuendelea.

Wakati huohuo, akijibu maswali ya waandishi wa habari waliokuwepo katika eneo hilo, Dk. Shein alisema uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika 20 Machi, mwaka huu, utakuwa huru na wa haki.

Kuhusu suala  la usalama,  Dk. Shein aliwahakikishia wananchi kuwa, amani na utulivu utaendelea kuwepo Unguja na Pemba na kuongeza kuwa, ulinzi na usalama wakati wote utaimarishwa ili wananchi wote wenye haki ya kupiga kura wafanye hivyo kwa mujibu wa katiba na sheria.

No comments:

Post a Comment