Sunday 6 March 2016

WAUGUZI WANATUMIA TOCHI KUZALISHA WAJAWAZITO

WAUGUZI katika zahanati ya kijiji cha Mwabomba, wilayani hapa mkoani Shinyanga, wanalazimika kutumia mwanga wa tochi ya simu wakati wa kuwazalisha kinamama wajawazito kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo.

Mganga Mkuu wa zahanati hiyo, Daniel Bukwimba, alisema hayo juzi, alipozungumza na waandishi wa habari waliofika kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili.

Dk. Bukwimba alisema wauguzi katika zahanati hiyo wamekuwa wakilazimika kutumia mwanga huo wakati wa usiku, wakati kinamama wanapokwenda kujifungua.

Alisema mbali na kukosa nishati ya umeme, bado zahanati hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo vifaa vya kupimia, uhaba wa vitanda vya kulala wagonjwa na dawa.

Kwa mujibu wa Dk. Bukwimba, zahanati hiyo inahudumia wagonjwa 30 hadi 40 kwa siku, huku kinamama wanaofika kujifungua ni watano hadi saba kwa siku, huku wauguzi waliopo ni watatu, ambao hawakidhi mahitaji ya wagonjwa.

“Tunaiomba serikali itusaidie kwa kutupatia wauguzi wengine kwani zahanati hii imekuwa na changamoto kubwa, hasa kwa kinamama wanaokuja kujifungua hapa, hasa wakati wa usiku.
Wanalazimika kutumia mwanga wa tochi za simu zao, jambo ambalo ni hatari katika kuokoa maisha ya mama na mtoto,”alisema.

Kwa upande wake, Diwani wa kata hiyo, Yuda Myalula, alisema zahanati hiyo inakabiliwa na changamoto ya nyumba za  watumishi wa afya, ambao  wanalazimika kuishi kwa muda kwenye vyumba vya zahanati na kwamba, zinazohitajika ni nyumba tano huku zilizopo ni mbili, walizopangishiwa kwa muda.

Katika kutatua changamoto hiyo, Myayula alisema  kijiji cha Mwabomba kimenunua eneo lenye ukubwa wa ekari nane, ambalo litatumika kujenga nyumba za watumishi pamoja na kupanua zahanati hiyo, ikiwemo ujenzi wa majengo ya utawala.

Naye mkazi wa kijiji hicho, Mashaka Charles, alisema eneo la Mwabomba lenye wakazi zaidi ya 50,000, kwa kiasi kikubwa hutegemea kupata huduma katika zahanati hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa, alitembelea zahanti hiyo na kujionea upungufu uliopo katika sekta ya afya, ambapo alitoa mifuko 100 ya saruji.

No comments:

Post a Comment