Sunday 6 March 2016

MPINA: HAKUNA KAMA MAJALIWA


NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Luhaga Mpina, amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amevunja rekodi ya utendaji kazi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.

Amesema Waziri Mkuu Majaliwa amefanya kazi kubwa na yenye tija kwa taifa, ikiwa ni pamoja na kusaidia kurudisha imani ya wananchi kwa serikali.

Amesema tangu alipoingia madarakani, amefanya kazi kubwa ya kushughulikia mafisadi, watumishi wasiokuwa na maadili pamoja na watu wanaokwepa kulipa kodi, jambo lililochangia kupandisha mapato ya serikali hadi kufikia sh. trilioni 1.4.

Mpina, ambaye ni Mbunge wa Kisesa, alisema hayo jana, katika Shule ya Sekondari ya Mwakaluba, iliyoko Kata ya Mwandoya, wakati Waziri Mkuu, Majaliwa alipokuwa akizindua maabara za masomo ya sayansi katika shule hiyo, akiwa katika siku yake ya nne ya ziara ya kikazi mkoani Simiyu.

Kwa mujibu wa Mpina, Majaliwa ameonyesha ujasiri mkubwa katika kushughulikia mafisadi na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi, jambo ambalo limeleta manufaa makubwa kwa taifa.

“Majaliwa amevunja rekodi ya utendaji kwa mawaziri wakuu nchini kwa sababu ana miezi mitatu tangu ateuliwe kushika wadhifa huu, lakini ameweza kufanya mambo makubwa tena kwa ujasiri mkubwa na tija imeonekana kwa wananchi na taifa kwa ujumla,”alisema.

Aidha, Mpina alimuomba Majaliwa kuwapatia fedha za ujenzi wa barabara inayoanzia Busega, Bariadi, Itilima, Meatu hadi Mkalama mkoani Singida, ili ijengwe kwa kiwango cha lami kwa kuwa ndiyo kiunganishi kikubwa cha maeneo hayo.

Pia, aliomba fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria, unaoanzia Busega, Bariadi, Dutwa, Itilima, Kisesa hadi Meatu, ambao utakapokamilika, utasaidia kumaliza changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa akizungumzia changamoto ya upatikanaji wa maji katika wilaya ya Meatu na mkoa mzima wa Simiyu, alisema mradi huo utatekelezwa.

Alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu, kuandika barua ya maelezo ili serikali iweze kupeleka fedha.

Alisisitiza kuwa miradi yote itakamilika kwa wakati kwa sababu fedha zipo na serikali itapeleka katika maeneo yote yenye mahitaji ili iweze kukamilika na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.

Kuhusu upungufu wa dawa na vifaa tiba kwenye hospitali na vituo vya afya, Majaliwa alisema serikali itapeleka dawa za kutosha na vifaa katika maeneo yote ya kutolea huduma za afya, lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Alimtaka mganga mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha dawa na vifaa tiba vitakavyopelekwa katika zahanati, vituo vya afya na kwenye hospitali ya wilaya, vinatumika kama ilivyokusudiwa na kutoa onyo kuwa wasiibe kwa sababu wakifanya hivyo, kitakachowapata anakifahamu.

No comments:

Post a Comment