Sunday 6 March 2016

RAIS MAGUFULI AONGOZA MAZISHI YA KAKA YAKE KIKWETE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimpa pole Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete kwa kufiwa na kaka yake, Mzee Selemani Mrisho Kikwete, wakati wa mazishi kijijini Msoga, Chalinze, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Machi 5, 2016PICHA NA IKULU

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akimfafanulia jambo  Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kabla ya mazishi ya Kaka yake Marehemu Mzee Selemani Mrisho Kikwete huko Msoga mkoani Pwani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Rais wa awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi  wakimsikiliza kwa Makini Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati akifafanua jambo huko Msoga Mkoani Pwani.

Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akiweka mchanga kwenye kaburi la Mzee Selemani Mrisho Kikwete huko Msoga mkoani Pwani. Mzee Selemani Kikwete alikuwa kaka mkubwa wa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan na Mama Janeth Magufuli, mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Mama Salma Kikwete wakiwa msibani kwa kaka yake Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, MarehemuMzee Selemani Mrisho Kikwete, wakati wa mazishi kijijini Msoga, Chalinze, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Machi 5, 2016. Wengine kutoka kushoto ni Mama Asha Bilali, Mama Khadija Mwinyi, Mama Sitti Mwinyi, Mama Asha Seif Ali Iddi,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akimfariji Mjane wa Marehemu Mzee Selemani Mrisho Kikwete, wakati wa mazishi kijijini Msoga, Chalinze, wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Machi 5, 2016
RAIS Dk. John Magufuli, amewaongoza maelfu ya wananchi kumzika Mzee Suleiman Kikwete, kaka wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Maziko ya Mzee Suleiman yalifanyika jana,  katika Kijiji cha Msoga wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo viongozi mbalimbali walishiriki.

Akitoa neno la shukrani kwa waliohudhuria maziko hayo, Rais mstaafu Kikwete alisema amefarijika na umati mkubwa wa waombolezaji waliojitokeza kumzika Mzee Suleiman.

Kikwete alisema kwa namna ya pekee, anamshukuru na kumpongeza Rais Dk. Magufuli kwa ushirikiano alioutoa wakati wa kumuuguza Mzee Suleiman na ushiriki wake kwenye maziko.

“Kwa namna ya pekee nasema asante sana Mheshimiwa Rais kwani ulilazimika kuchukua uamuzi mgumu ili kuhakikisha mzee wetu anapata matibabu,” alisema.

Kwa mujibu wa Kikwete, walipotaka kumpeleka Mzee Suleiman nchini India kwa ajili ya matibabu ya maradhi ya kansa yaliyokuwa yakimsumbu, Dk. Magufuli alilazimika kuamuru ubalozi wa nchi hiyo nchini kufunguliwa Jumapili ili utoe viza kwa ndugu waliokuwa wakimpeleka nchini humo kwa ajili ya matibabu.

Alisema mbali na ubalozi huo pia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Seif, aliamuru Idara ya Uhamiaji kufanya kazi usiku ili kuwaongezea muda hati za kusafiria, Mohammed Kikwete na Khalfan Kikwete, waliokuwa wakimsindikiza Mzee Suleiman.

“Kwa haya yote nasema asante kwa niaba ya familia yetu kwa ushirikiano uliotupa kumsaidia Mzee Suleiman, ambaye alikuwa ni msaada mkubwa kwangu na familia yetu kwa jumla,” alisema.

Mbali na  Dk. Magufuli, maziko hayo yalihudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,  marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na mawaziri wakuu wastaafu, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi.

Mzee Suleiman alizaliwa Februar, 1936, akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto tisa wa Mzee Mrisho Kikwete.

Wakati huo huo, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuiwakilisha vyema nchi kwenye kikao cha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC).

Kikwete alisema hayo jana, alipokuwa akitoa shukurani kwa waliohudhuria maziko ya kaka yake, marehemu Mzee Suleiman Kikwete.

Alisema Dk. Magufuli ameidhihirishia dunia kwamba Tanzania haikukosea kumchagua kwenye nafasi hiyo. “Nakupongeza sana mheshimiwa Rais, uwakilishi wako umekuwa wa mafanikio makubwa, endelea na kasi hiyo hiyo,” alisema.

Katika mkutano  huo wa wakuu wa nchi za jumuia hiyo, uliofanyika Arusha, Dk. Magufuli alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa EAC.

No comments:

Post a Comment