Sunday 6 March 2016

SERIKALI KUMLIPA FIDIA MWEKEZAJI BIL. 10/-

SERIKALI imesema itamlipa fidia ya sh. bilioni 10, mwekezaji wa Kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill, kufuatia wananchi kuvamia eneo lake.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema hayo juzi, alipozungumza na wananchi wa Chasimba, Kata ya Wazo, Dar es Salaam.

Lukuvi alisema serikali imeridhia kumlipa mwekezaji huyo, kufuatia wananchi wa Chasimba, Chatembo na Chachui kuvamia eneo hilo miaka mingi.

“Eneo mlilovamia ni ekari 224, mwekezaji aliwashinda mahakamani, lakini serikali imeamua kuwasaidia kwa kumsihi tumpatie fidia ili awaache muendelee kuishi eneo hili, hivyo tunaanza kupima, kupanga na kuwamilikisha,”alisema.

Hata hivyo, Lukuvi alisema mpango huo utawahusu wananchi waliojenga ama kununua maeneo hayo kabla ya mwaka 2012, kabla ya mgogoro huo, ambapo serikali ilisitisha shughuli za ununuzi, uuzaji na uendelezaji wa maeneo hayo.

Aliwataka wananchi hao kuchangia gharama za upimaji ambapo fedha za malipo ya awali, zaidi ya asilimia saba ya thamani ya eneo husika, itafunguliwa akaunti maalumu ijulikanayon kama ‘Escrow Account’, ambapo fedha hizo pia zitasaidia kumlipa fidia mwekezaji.

Waziri huyo alisema vitapimwa viwanja 4,000 katika kata hiyo, ambapo aliwataka kuendelea kuheshimu makubaliano ya kutokuchimba wala kuuza mawe ya chokaa katika eneo hilo.

Pia, alisema shughuli ya kupima, kupanga na kumilikisha maeneo hayo itaanza rasmi wiki ijayo

Katika mkutano huo, Waziri Lukuvi alizindua mpango wa urasimishaji kata za Kimara na Saranga, wilayani Kinondoni, kama eneo la mfano wa upangaji miji, ili kuwawezesha wananchi kuwa na makazi yaliyopangwa na kurahisisha ukusanyaji wa mapato.

Alisema wananchi waliojenga katika kata za Kimara na Saranga, kabla serikali haijaanzisha utaratibu wa kupima maeneo, waathirika watafikiriwa namna ya kufidiwa.

“Tunaomba ushirikiano katika mpango huu kwani shughuli ya upimaji, hususan maeneo itakayopita miundombinu, itaanza wakati wowote kuanzia sasa na maeneo yote yaliyokuwa mashamba, yatapimwa viwanja,” alisema.

Alisema baada ya eneo hilo kupimwa, zitatolewa hatimiliki kwa kipindi cha mwezi mmoja, ambapo wahusika watatakiwa kulipia hati hizo huku wasiojiweza kifedha watapewa kipindi cha mwaka mmoja kulipa taratibu hadi watakapochukua hati zao.

Lukuvi alisema shughuli hiyo itawahusu waliojenga kwenye maeneo salama kwa mujibu wa sheria ya mazingira na si yaliyokatazwa na serikali, yakiwemo ya wazi, mabondeni na pembezoni mwa kingo za mito.

“Nawataka wananchi wa kata hizi kuwa na utayari kwa usumbufu mtakaoupata kwa kuwa baadhi yenu mtapoteza mali, ikiwemo ardhi na nyumba, hususani maeneo itatakayopita miundombinu ya umeme, maji, barabara na zitakapojengwa huduma za jamii kama shule na zahanati,” alisema.

Alisema ramani itakayotumika sasa katika eneo hilo itakuwa ya kudumu katika mpango mkuu wa jiji la Dar es Salaam, unaotarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Lukuvi alisema eneo hilo lina wakazi zaidi ya 88,000 na serikali inatarajia kupima jumla ya viwanja 22,000 na kuwataka wananchi baada ya kukamilika urasilishaji, wahakikishe wanalipa kodi za ardhi na majengo kwa ajili ya maendeleo yao.

Alisema urasimishaji huo utasaidia kudhibiti ujenzi holela, migogoro ya ardhi na kupanua wigo wa ukusanyaji mapato ya serikali.

No comments:

Post a Comment