Tuesday 24 May 2016

17 WAKAMATWA KWA KUSAFIRISHA BIDHAA ZA MAGENDO


SERIKALI imesema jumla ya wafanyabiashara 17, wamekamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani baada ya kukamatwa wakisafirisha bidhaa kwa njia ya magendo.

Imesema wafanyabiashara hao walikamatwa kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, kutokana na doria iliyofanywa majini na vyombo vya usalama.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, alisema hayo bungeni mjini hapa jana, alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge Maryam Msabaha (CHADEMA).

Katika swali lake, mbunge huyo alitaka kujua mkakati wa serikali katika kuwadhibiti wafanyabiashara wasio waaminifu, wanaotumia bandari bubu na kukwepa kodi.

Pia alitaka kujua ni wafanyabiashara wangapi waliokamatwa katika bandari bubu na kufikishwa mahakamani.

Ngonyani alisema mwaka jana, msako huo wa polisi uliwawezesha kuwakamata wafanyabiashara 81, waliokuwa wakisafirisha bidhaa hizo kwa njia haramu.

Alisema katika msako huo, bidhaa nyingi zilikamatwa na kutokana na wamiliki wake kutofahamika, zimetaifishwa na serikali.

Ngonyani alizitaja bandari bubu zilizorasimishwa katika mwambao wa bahari ya Hindi kwa upande wa Tanzania Bara kuwa ni Mbweni, Pwani-Mlingotini, Kisiju na Nyamisati.

Kwa mkoa wa Tanga, alizitaja bandari hizo bubu kuwa ni Jasini, Kigombe, Kipumbwi, Mkwaja na Pangani; Mtwara ni Kilambo na kwa mkoa wa Lindi ni Rushingi na Kilwa Kivinje.

“Utaratibu wa kurasimisha bandari binafsi umefanyika katika Ziwa Victoria, Halmashauri ya Ilemela na Nyamagana, Mwanza,” alisema.

Alibainisha kuwa bandari tisa binafsi zimetambuliwa na kuimarishwa na kwamba, utaratibu huo utaendelea pia katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa.

Alisema serikali inatambua uwepo wa wafanyabiashara wasio waaminifu, wanaotumia bandari bubu kupitisha biashara za magendo, dawa za kulevya, maliasili, uhamiaji haramu, uvuvi haramu na matumizi ya vyombo vya majini visivyo salama ili kukwepa kodi na pia kuhatarisha usalama wa nchi.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi, Hamad Yusuph Masauni, amekiri vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliwa na changamoto kubwa wakati wa kupambana na uharifu, vinapofanya doria majini.

Masauni alieleza hayo bungeni mjini hapa jana, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Maryam Msabaha (CHADEMA).

Katika swali lake, Maryam alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuvipatia vifaa vya kisasa vyombo vya ulinzi na usalama vinavyofanya kazi ya kudhibiti vitendo vya uharifu majini, ambavyo vimekuwa vikikumbwa na changamoto kubwa kwa kukosa vitendea kazi.

Naibu waziri alisema serikali imekuwa ikiimarisha doria za majini, ikiwa ni pamoja na kuwapatia vifaa vya kisasa askari wanaofanya doria katika maeneo hayo.

Alisema serikali itaendelea na jitihada za kuwapatia vifaa vya kisasa kila mara, kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

No comments:

Post a Comment