Saturday 7 May 2016

MAHAKAMA KUU YATUPILIA MBALI RUFANI YA DPP


Na JacquilineMrisho - MAELEZO

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyokuwa ikipinga kuondolewa kwa shitaka la 8 la utakatishaji fedha linalomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Harry Kitilya na wenzake wawili.

Uamuzi huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Moses Mzuna alipokuwa akitoa majibu ya rufaa iliyokuwa imekatwa na DPP.

“Ninafahamu kila kesi inaamuliwa kutokana na mazingira yake lakini nimefuta rufaa hii kwa kuwa hoja zilizotolewa hazina nguvu kisheria” alisema Jaji Mzuna.

Aidha Jaji Mzuna amefafanua kuwa hata kama amefuta rufaa hiyo lakini upande wa Jamuhuri bado una nafasi ya kubadilisha shitaka au hati nzima ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Timony Vitalis amekubaliana na uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo juu ya pingamizi lake ingawa bado anasimamia watuhumiwa kutofutiwa shitaka la utakatishaji wa fedha.

Naye Wakili wa Utetezi Majula Magafu amesema kuwa wao wanasubiri maamuzi yatakayotolewa na Wakili wa Serikali ili wajue namna ya kuikabili kesi hiyo.

No comments:

Post a Comment