Wednesday 1 June 2016

KIBAJAJI AWASHUKIA WABUNGE WA UPINZANI


MBUNGE wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde 'Kibajaji', amewashutumu wabunge wa kambi rasmi ya upinzani kwa kuendekeza hoja zisizokuwa na maslahi bungeni, ikiwemo kukejeli juhudi zinazofanywa na serikali katika kubana matumizi ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, amelazimika kufuta baadhi ya maneno ya hotuba ya kambi ya upinzani, kwenye kumbukumbu ya taarifa za bunge, kutokana na maneno hayo kujaa maneno ya uchochezi, maudhi na yenye ukakasi.

Hotuba hiyo ya upinzani ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda, iliyowasilishwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ilikuwa na maneno yaliyoelezwa yalikuwa na msingi wa uchochezi.

Maneno ambayo Chenge aliamua yafutwe yalikuwa yakisomeka: 'Uhusiano mzuri wa kimataifa wa nchi yeyote ile duniani, unategemea ustaarabu wa ndani na mwenendo mzuri wa serikali ya nchi hiyo kwa watu wake.'

“Nchi yenye serikali katili ya kidiktekta, isiyopenda kukosolewa, ya kifisadi, isiyoheshimu haki za binadamu, utawala wa sheria, demokrasia na inayokandamiza uhuru wa wananchi wake kama Tanzania, haiwezi kuheshimiwa wala kuwa kivutio kwa mataifa mengine katika kujenga na kudumisha uhusiano mzuri na wenye tija kimataifa.'

Kutokana na maneno hayo, Chenge alisema kwa mujibu wa kanuni ya tano, fasiri ya kwanza ya kanuni za bunge, maneno hayo yaondolewe na yasiwe sehemu ya taarifa rasmi za bunge.

Alisema maamuzi hayo ameyafikia kwa kuzingatia maamuzi ya nyuma ya maspika kama inavyotakiwa.

Baada ya uamuzi huo, Chenge aliendelea na shughuli za bunge kwa kumuita Lusinde kuanza kuchangia hoja ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Katika mchango wake, Lusinde alieleza kushangazwa na namna hotuba ya kambi ya upinzani ilivyopandikwa kwa maneno yasiyofaa, ikiwemo jina la Mungu kuandikwa kwa herufi ndogo badala ya kubwa, kitendo kilichoashiria namna kambi hiyo inavyoendesha mambo yake kwa mtindo wa kipekee.

Alisema madai yaliyotolewa na kambi hiyo kuwa serikali ni ya kifisadi, hayana msingi kwa sababu fisadi mkuu yuko kwenye kambi ya upinzani.

“Mnanishangaza kwa kweli, eti serikali ya kifisadi wakati huyo fisadi mkuu mnaye nyie kwenye kambi yenu.

“Hawa watu walikuwa wakimsema Rais Jakaya Kikwete, kuwa anasafiri kila siku, lakini leo Rais Dk. John Magufuli, ameanza kubana matumizi kwa kutosafiri, eti wanadai anaogopa, hivi nyie ni watu wa aina gani?” Alihoji Lusinde.

Alisema hapa nchini wapo wapinzani dhaifu wasiokuwa na uwezo hata wa kujenga hoja, ambao kazi yao ni kupinga kila jambo.

Aliongeza kuwa wapinzani wamekuwa wakiondoka bungeni bila kufanyakazi,  hivyo kipindi kijacho cha uchagazi hakutoweko upinzani kutokana na kasi ya uchapakazi ya Rais Magufuli kuendelea kukubalika ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge wamesema adhabu waliyopewa wabunge wenzao inastahili kwa sababu wamekiuka sheria, kanuni na taratibu za bunge.

Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mbunge wa Buchosa (CCM), Dk. Charles Tizeba, alisema adhabu waliyopewa wabunge hao inastahili kwa sababu wamesahau kuwa bunge linaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu.

“Haiwezekani wabunge wafanye mambo kwa kujiamria wenyewe na kuvunja sheria na kanuni kwa kufanya vurugu na bado kiti (spika) aendelee kuwafumbia macho, hivyo adhabu waliyopewa ni sahihi,” alisema.

Dk. Tizeba alisema wabunge wanatakiwa kukumbuka kuwa adhabu hiyo si kwa ajili ya CHADEMA pekee, bali kwa wabunge wote ambao watavunja sheria na kanuni za bunge.

Kwa upande wake, Jasson Rweikiza (Bukoba Vijijini-CCM) alisema bunge ni mahala pa kufanyakazi kwa umakini na kujenga hoja na wala si kufanya vurugu au kupiga kelele.

“Lazima tufuate kanuni na sheria zilizowekwa na si kupiga kelele. Kama kuna kitu mbunge hajakubaliana nacho, anatakiwa kujenga hoja ili kukishawishi kiti (spika) kimsikilize tena kwa hoja na si kufanya fujo,” alisema.

Dk. Hamis Kigwangalla (Nzega Vijijini-CCM), alisema adhabu waliyopewa wabunge hao ni sahihi kwa sababu waliitwa na kuhojiwa na kukutwa na makosa, hivyo kanuni na sheria zilifuatwa.

“Waliitwa na kamati na kuhojiwa na kila mmoja alivyohojiwa alikutwa na makosa, ingawa yanatofautiana na hivyo kila mmoja amehukumiwa kutokana na kosa alilotenda,” alisema.

No comments:

Post a Comment