Wednesday 1 June 2016

WABUNGE UKAWA WAMSUSIA VIKAO NAIBU SPIKA

WABUNGE wa kambi rasmi ya upinzani (UKAWA), wameendeleza vituko vya kususia vikao vya bunge, ambapo mara hii wameamua kutohudhuria vikao vyovyote vya bunge, vitakavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Akson.

Uamuzi huo wameuchukua kutokana na madai kwamba, Dk. Tulia amekuwa akiendesha vikao vya bunge pasipo kujali maoni yao.

Wabunge hao jana, waligomea kuhudhuria kipindi cha maswali na majibu kilichoendeshwa na Naibu Spika.

Licha ya kufikia uamuzi huo, baadhi ya wananchi na wanasiasa wameeleza kuwa, uamuzi huo una athari kwa kambi yao pamoja na wananchi wanaowawakilisha.

Hata hivyo, wengine wamedai kuwa huo ni utamaduni uliojengeka kwenye mabunge ya Jumuia ya Madola, kwa wabunge kutoka nje pindi wanapokuwa hawakubaliani na hoja au uamuzi.

Akizungumzia uamuzi huo, Mwenyekiti wa kambi hiyo, Freeman Mbowe, alisema hawatahudhuria vikao vitakavyoendeshwa na Dk. Tulia hadi atakapotambua umuhimu wao.

Alisema watakutana na wabunge, ambao juzi walisimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge, kutokana na kukutwa na makosa ya kufanya vurugu bungeni Januari 27, mwaka huu, ili kupeleka malalamiko yao kwa wananchi bila kujali vyama wanavyotoka.

Mbowe alisema hawawezi kukubali kumuona naibu spika anaridhia kufukuzwa kwa wabunge hao.

Akijibu swali kuhusiana na athari watakazozipata kisiasa kwa kutowawakilisha wananchi kwenye vikao vya bunge vitakavyoendeshwa na Dk. Tulia, alisema hakuna demokrasia isiyokuwa na gharama.

“Kila jambo unalolipeleka kwa wananchi lina gharama, hivyo tunapokubali kufanya maamuzi hayo tumekuwa tukiridhia, hivyo hatutasumbuka kuingia bungeni endapo tutamuona naibu spika akiendesha vikao,” alisema.

Akizungumzia uamuzi huo wa wabunge wa upinzani, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Twaha Taslima, alisema  muathirika wa kwanza wa uamuzi huo ni yule anayetoka bungeni licha ya utamaduni huo kuwa sehemu ya mabunge ya Jumuia ya Madola.

Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu John, kampasi ya Dar es Salaam, Eston Ngilangwa, alisema kabla ya kufikiwa kwa maamuzi hayo, ni vyema maslahi ya wananchi yangewekwa mbele.

Aliongeza kuwa wabunge ndiyo wawakilishi wa wananchi, hivyo kugomea vikao vya bunge, kutasababisha wananchi kukosa kuwakishwa kwa matatizo yao ya msingi.

Mwamalanga Emmanuel, mkazi wa Kongwa mkoani Dodoma, alisema wabunge wa wapinzani hawakupaswa kugomea vikao vya bunge kwa sababu wao ndio waliokuja kwa wananchi kutaka kuwawakilisha bungeni.

Alisema kama walifahamu kwamba wakiingia bungeni watagombea kuhudhuria vikao hivyo, ni vyema wasingejitokeza kuomba nafasi hiyo ya uwakilishi kwa wananchi.

Juzi, bunge liliridhia kusimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge kuanzia Machi 30, mwaka huu, wabunge saba wa kambi ya upinzani, baada ya kubainika kudharau mamlaka ya spika kwa kufanya fujo bungeni, licha ya kutakiwa kutokufanya hivyo kwenye kikao cha bunge cha Januari 27, mwaka huu.

Akisoma maamuzi hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge, Kepteni George Mkuchika, aliwataja wabunge hao kuwa ni Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na Tundu Lissu wa Singida Mashariki, ambao hawatahudhuria vikao vilivyosalia vya mkutano wa tatu wa na vikao vyote vya mkutano wa nne wa Bunge la 11.

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekur, Godbless Lema wa Arusha Mjini, John Heche na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambao hawatahudhuria vikao vilivyosalia vya mkutano wa tatu wa bunge la 11.

No comments:

Post a Comment