Sunday 26 June 2016

NAIBU SPIKA DK. TULIA ASHIRIKI HARAMBEE YA KUWACHANGIA WANAHABARI


 Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson Mwansasu katika tukio la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya waandishi wa habari nchini tukio hilo lilifanyika jana katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma. Katika tukio hilo Dk. Tulia Ackson alichangia kiasi cha shilingi milioni moja.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson Mwansasu (kushoto), Msanii wa Bongo Movie, Aunt Ezekiel (kulia) na Miss Tanzania 2014/15, Lilian Kamazima (katikati) wakiosha moja ya magari ya wabunge na wadau wengine kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya waandishi wa habari nchini.


Na Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Naibu Spika Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameshiriki harambee ya kuchangia waandishi wa habari kwa ajili ya kuwakatia Bima ya Afya “Media Car Wash For Health” iliyofanyika leo katika viwanja vya Jamhuri Mjini Dodoma ambapo amechangia jumla ya shilingi milioni 5 ili kuokoa maisha ya waandishi wa habari.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuwachangia waandishi wa habari kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya nchi na kuhamasisha amani ya nchi, kwa kutambua umuhimu wao nitachangia shilingi 5,000,000 ili iweze kuwakatia Bima ya Afya,” alisema Mhe.Dkt. Tulia.

Licha ya kuchangia fedha hizo Mhe. Tulia aliosha baadhi ya magari ya waheshimiwa wabunge kwa ajili ya kuchangia harambee hiyo ambapo kila mbunge aliyeoshewa gari yake alichangia shilingi 100,000 ambazo moja kwa moja ziliingia katika mfuko wa kuokoa maisha ya waandishi wa habari kwa kuwakatia Bima ya Afya.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendelea ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Hamis Kigwangalla amechangia shilingi 1,000,000/= ambayo nayo inaenda kusaidia waandishi wa habari ili waweze kukatiwa Bima ya Afya.

Lengo la harambee hiyo ni kukusanya zaidi ya shilingi milioni 200 ambazo zitatumika kuwakatia Bima ya afya zaidi ya  waandishi wa habari 1000 hapa nchini.  Aidha harambee hii ni ya pili, harambee nyingine kama hii ilifanyika mwaka 2015, viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukusanya shilingi milioni 30 ambazo zilisaidia kugharamia matibabu kwa waandishi watatu waliokuwa wanaugua kwa kipindI kirefu.

No comments:

Post a Comment